2018-07-22 14:32:00

AMECEA: Wekezeni katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani


Kanisa Barani Afrika halina budi kuwekeza katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, yanayojikita katika kukidhi mahitaji msingi ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kuheshimu haki zake msingi, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ni maendeleo ya watu na wala si vitu; ni maendeleo yanayogusa utu, ustawi na mafao ya wengi.

Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kuyafahamu vyema Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuyamwilisha katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji, kwa kukazia: utu wa binadamu, mshikamano unaoongozwa na kanuni auni pamoja na mafao ya wengi. Haya ni mambo msingi yanayoongoza na kuratibu shughuli za Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kama yalivyofafanuliwa na Monsinyo Bruno Marie Duffè, Katibu mkuu wa Baraza hili wakati akishiriki kwenye mkutano wa 19 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”.

Dhana ya maendeleo endelevu inajikita katika mchakato mzima wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kuangalia vipaumbele na mahitaji msingi ya binadamu na wala si kutaza soko la dunia. Huu ni mchakato wa ujenzi wa sanaa ya kusikiliza na kusikilizana; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema katika masuala ya kiuchumi; kwa kutumia vyema rasilimali fedha na watu katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujizatiti kikamilifu, ili kukabiliana na changamoto za athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, ili kukuza na kudumisha mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni ili hatimaye, kutangaza na kushuhudia Injili ya amani Barani Afrika kama chachu ya maendeleo endelevu na fungamani kwa watu wa Mungu!

Umefika wakati kwa Kanisa Barani Afrika kuwekeza zaidi katika miradi yenye mvuto na mashiko ya kijamii: kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto hii inaweza kufikiwa ikiwa kama kutakuwepo na ushirikiano kati ya nchi za AMECEA na SECAM pamoja na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya, hali ngumu ya uchumi na ukata kwa familia nyingi Barani Afrika, vita na kinzani za kisiasa, kidini na kijamii ni kati ya mambo yanayokwamisha utekelezaji wa Injili ya matumaini kwa familia ya Mungu Barani Afrika. Ikumbukwe kwamba, uinjilishaji wa kina unagusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, dhana ambayo ilifanyiwa kazi sana na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Monsinyo Bruno Marie Duffè amekaza kusema, Bara la Afrika leo hii linakabiliwa na changamoto kubwa ya wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, lakini, hawa ni watu wanaokumbana na hali ngumu na tete katika maisha yao. Haya ni matokeo ya vita, kinzani na nyanyaso za kidini, kikabila na kisiasa. Kuna umaskini mkubwa wa hali, kipato na maadili. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba,  kuna zaidi ya watu milioni 5, 472, 000 ambao hawama makazi ya kudumu kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii Barani Afrika. Zaidi ya watu milioni 2, 561, 000 wanakimbia makazi na nchi zao kutokana na majanga asilia. Maeneo yaliyoathirika sana ni Sudan ya Kusini, Somalia, Ethiopia na Uganda.

Changamoto zote hizi zinaweza kuvaliwa njuga na familia ya Mungu Barani Afrika kwa: kujikita katika mshikamano, umoja na udugu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kuwekeza katika elimu bora na makini kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote na kubwa zaidi, kukataa kumeng’enyuliwa kwa udini, ukabila na itikadi ambazo mara nyingi ni kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache wenye uchu wa mali, madaraka na sifa. Kanisa Barani Afrika linapaswa pia kuongoka na kuambata maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; kwa kujikita katika kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.

Bara la Afrika halina budi kuendelea kuthamini, kujali na kutunza utu na heshima ya wanawake Barani Afrika wanaochangia sana katika ustawi, maendeleo na familia ya Mungu Barani Afrika, lakini bado wananyanyasika sana. Kumbe, ushuhuda wa kweli za Kiinjili na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii ziendelezwe na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kuna pengo kubwa kati ya matajiri na maskini, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, hali inayopelekea pia kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini, kisiasa na kikabila, lakini waathirika ni raia wa kawaida.

Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia umeugeuza dunia kuwa kama kijiji, kuna faida zake, lakini pia kuna athari zake kubwa hasa kwa vijana wa kizazi kipya, ambao wanaendelea kutumbukia katika ombwe la kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, kwa kung’olewa kutoka katika tamaduni, mila na desturi zao njema na kuanza kuiga mitindo na maisha ya kigeni yasiyokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya vijana Barani Afrika. Kumbe, wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu washirikiane, ili kuibua mbinu mkakati utakaoleta matumaini kwa familia ya Mungu Barani Afrika.

Uchu wa mali, utajiri wa haraka haraka, udini na ukabila ni kati ya mambo ambayo yanachangia vita, kinzani na mipasuko ya kijamii katika Nchi za AMECEA. Kumbe, Kanisa halina budi kuwa ni chombo na shuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu anasema Monsinyo Bruno Marie Duffè. AMECEA katika ujumla wake, inaonekana kujielekeza zaidi katika kukabiliana na changamoto zote hizi katika mwanga wa Injili, ukweli na uwazi na kwamba, Kanisa halina budi kuwa ni chombo cha maendeleo endelevu na fungamani kwa binadamu, hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa litaendelea kutekeleza utume wake kama chombo cha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano, mambo msingi yaliyopembuliwa kwa kina na mapana na Mababa wa AMECEA katika mkutano wao wa 19 huko Addis Ababa, Ethiopia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.