2018-07-19 15:06:00

Kanisa Barani Afrika halina budi kujielekeza katika kujitegemea zaidi


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, limeidhinisha kiasi cha dola milioni 1.4 kwa ajili ya kugharimia miradi 54, kama kielelezo cha mshikamano katika huduma na utekelezaji wa miradi ya shughuli za kichungaji Barani Afrika. Hii ni fedha ambayo imetolewa kwenye Mfuko wa Mshikamano na Kanisa la Bara la Afrika. Kati ya nchi zitakazofaidika na fedha hii ni pamoja na Kituo cha Radio Maria, Lesotho, kwa ajili ya kusaidia kuboresha matangazo yake, ili yaweze kuwafikia watu wengi zaidi. Fedha hii itatumika kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya kurushia matangazo.

Msaada huu umetolewa pia kwa Jimbo Katoliki la Wa, lililoko nchini Ghana, kwa ajili ya kuanzisha ofisi maalum ya kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Lengo ni kuanzisha utamaduni utakaowashirikisha watu wote katika dhamana na utume wa kuwalinda watoto na kuwasaidia katika malezi na makuzi yao: kiroho na kimwili. Msaada huu, utaliwezesha Jimbo kuandaa semina mbali mbali kwa ajili ya walinzi wa watoto Kijimbo na Kishule, dhamana ambayo kwa sasa inaelekezwa zaidi kwa wakleri na watawa. Jimbo Katoliki la Wa linataka kuunda mazingira rafiki yatakayowawezesha watoto kukua na kukomaa pasi na nyanyaso. Watoto wanatarajiwa pia kupewa mbinu za maendeleo, pamoja na kulisaidia Jimbo kutengeneza sera na mbinu mkakati kwa ajili ya ulinzi wa watoto wadogo mintarafu sheria za nchi kuhusu ulinzi wa watoto nchini Ghana.

Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda linaendeleza mchakato wa upatanisho, haki na amani, kufuatia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Maaskofu wanataka kuwajengea watu uwezo wa kuwasiliana moja kwa moja kwa lugha ya Kinyarwanda. Hii ndiyo lugha ambayo itatumika kwenye shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Rwanda, ili hatimaye, kuweza kujenga na kudumisha utamaduni wa umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu nchini Rwanda na kwamba, tofauti zao za kikabila, ni utajiri na amana inayopaswa kudumishwa na wala kisiwe ni chanzo cha maafa na mauaji ya kimbari kama ilivyojitokeza katika historia ya nchi hii.

Kardinali Joseph William Tobin wa Jimbo kuu la New Jersey, Marekani, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kwa ajili ya Bara la Afrika anasema, ruzuku ya maendeleo kwa Kanisa Barani Afrika ni ushuhuda wa mshikamano katika mchakato wa kutaka kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho na kwamba, Wakristo Barani Afrika wanapaswa kuwa ni mashuhuda na wajumbe wa Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Msaada huu pia unalenga kusaidia mchakato wa malezi na majiundo awali na endelevu kwa mihimili ya uinjilishaji Barani Afrika; uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuhimiza tunu msingi za maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo bila kusahau jitihada za kuwaandaa viongozi walei ili wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Fedha hii ni mchango unaotolewa na waamini wa Kanisa Katoliki pamoja na watu wenye mapenzi mema kutoka nchini Marekani. Mababa wasisi wa AMECEA waliwahi kusema, kati ya mbinu mkakati unaopaswa kuvaliwa njuga ni kulitegemeza Kanisa Barani Afrika. Jambo hili limerudiwa tena na Padri Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu wa AMECEA wakati wa ufunguzi wa Mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA unaoendelea huko Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe 13 hadi 23 Julai 2018. Anasema, AMECEA ilizaliwa kwa lengo la kuwa na mbinu za pamoja  za kichungaji kwa maslahi ya watu wa kanda ya AMECEA. Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa ni kuimarisha imani Katoliki na maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kwa kuwa na Mpango Mkakati  wa muda mrefu  uliowekwa katika Mkutano  Mkuu wa AMECEA uliofanyika Julai 1961, kwenye Ukumbi wa Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar es Salaam ukiwa na  dhamira kuu ya  “Kesho ya Kanisa la Bara la Afrika.” Kujitegemea na kulitegemeza Kanisa ni changamoto pevu kwa wakati huu.

Kardinali Joseph William Tobin katika hotuba yake, kwenye mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA unaoendelea huko Addis Ababa nchini Ethiopia ameitaka familia ya Mungu Afrika Mashariki kutembea na kusindikizana katika umoja, haki, upendo na mshikamano wa dhati sanjari na kushirikiana katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Afrika Mashariki na Kati. Kwa maneno mengine, huu ni wakati wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.