2018-07-13 16:03:00

Viongozi wa Kidini Kenya wasema, rushwa ni janga la kitaifa!


Rushwa na ufisadi vinaanza kumpekenyua mwanadamu kwanza kabisa katika maisha ya kiroho, yaani kutoka katika undani wa mtu mwenyewe na kupanua wigo huu katika maisha ya kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi. Mama Kanisa anawajibu na dhamana katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, saratani inayoleta taabu sana katika maisha ya mataifa mengi duniani, kiasi cha kukwamisha: haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Hii ni changamoto pevu katika maisha, utume na utambulisho wa Kanisa, ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu kuhusu “Rushwa” kilichotungwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu baada ya kufanya mahojiano na Bwana Vittorio V. Albert. Kardinali Turkson anasema, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; uhalifu wa magenge kitaifa na kimataifa. Ili kufanikisha mapambano haya, rushwa haina budi kushughulikiwa kama “Mbwa koko” ndani ya Kanisa kwa kujikita katika: kanuni maadili, utu wema sanjari na kuambata tunu msingi za Kiinjili.

Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuongoza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Lakini kwanza kabisa, Kanisa halina budi kuwa safi pasi na mawaa wala makunyanzi ya rushwa na ufisadi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, rushwa ni mchakato unaoharibu na kuvunjilia mbali kabisa mafungamano,upendo na mshikamano wa binadamu. Rushwa inatia doa uhusiano kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji. Lakini kinyume cha rushwa ni: Uaminifu, uadilifu, utu wema, upole na unyofu wa moyo mambo yanayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Nchini Kenya, Jukwaa la Majadiliano ya Kitaifa linaloundwa na Viongozi wa Kidini nchini Kenya, hivi karibuni, limemwomba Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kutamka wazi kwamba, rushwa na ufisadi ni janga la kitaifa nchini Kenya, kutokana na ukweli kwamba, rushwa na ufisadi imekuwa ni saratani ya hatari sana inayopekenyua sekta mbali mbali za maisha nchini Kenya. Umefika wakati kwa Serikali kufanya maamuzi magumu katika mapambano dhidi ya rushwa ili hatimaye, Kenya iweze kuanza kuandika historia mpya ya maisha ya watu wake bila kuchafuliwa na rushwa. Jukwaa la Viongozi wa Kidini nchini Kenya, wametoa tamko hili hapo tarehe 4 Julai 2018 huko kwenye Ukumbi wa Ufungamano, Jijini Nairobi.

Itakumbukwa kwamba, tamko hili ni sehemu ya mchakato wa viongozi wa kidini nchini Kenya wanaotaka kukoleza majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Kenya kufuatia machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza hivi karibuni nchini Kenya wakati na mara baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika mwaka 2017. Askofu mkuu Martin Musonde Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa na Mheshimiwa Canon Peter Karanja, Makamu Mwenyekiti ambaye pia ni Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Kenya, NCCK. Viongozi hawa wanaitaka Serikali kupitisha Sheria itakayotoa msamaha kwa wale wote “waliokwapua vigunia vya fedha ya umma” na kuamua kuvirejesha tena Serikalini; pamoja na kutoa adhabu kali kwa wala rushwa na mafisadi wa mali ya umma, ili iweze kuwa fundisho kwa wote wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka; mambo yanayolitumbukiza taifa kwenye majanga makubwa!

Jukwaa la Majadiliano ya Kitaifa nchini Kenya linapenda kujielekeza zaidi katika masuala mtambuka na tete yanayogusa kwa karibu sana maisha ya wananchi wengi wa Kenya. Ni Jukwaa linalotaka kuona ufanisi katika huduma za kijamii zinazotolewa na Serikali; mageuzi katika sekta ya ulinzi na usalama wa raia; maboresho ya Katiba, Sheria za Nchi pamoja na kuhitimisha malumbano yaliyojitokeza mara baada ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2017.

Viongozi wa kidini pia wanaiomba Serikali kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi wake kwani Bajeti ya mwaka 2018 imeongeza kodi kubwa ambayo inalalamikiwa na watu wengi, kwani inachangia kuwatumbukiza wananchi wa kawaida katika dimbwi la umaskini! Viongozi wa kidini wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, bidhaa zinazoingizwa nchini humo zinazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa na kwamba, bidhaa zilizopitwa muda na zenye viwango hafifu zisiruhusiwe kuingia wala kuuzwa nchini Kenya.

Askofu Peter Kihara Kariuki wa Jimbo Katoliki la Marsabit ameitaka familia ya Mungu nchini Kenya, kuwa ni mashuhuda wa huruma, upendo na mshikamano; kwa kuguswa na mahitaji ya jirani zao. Wawe makini kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha: umoja, usawa na mapendo ili kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi, unatumika kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Kutokana na saratani ya rushwa, imekuwa ni vigumu sana wananchi wengi kupata maendeleo endelevu. Askofu Kariuki anakaza kusema, anasema, utajiri wa Kenya unamilikiwa na watu wachache, wakati kuna wimbi kubwa la wananchi ambao wanateseka sana kupata mahitaji yao ya kila siku! Umaskini wa hali na kipato unaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa nchini Kenya.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, rushwa inaonesha maisha ya mwanadamu asiyekuwa na  dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayoharibu sana mafungamano ya kijamii. Matokeo yake ni kukomaa kwa ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko; tabia ya kutowajali wengine. Rushwa inaonesha ile roho ya korosho, roho ya kwa nini; roho ya kutu, roho iliyovunda na kuanza kutoa harufu mbaya. Rushwa ni kikwazo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inapelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Ni chanzo kikuu cha kuibuka na kusambaa kwa magenge ya kihalifu, kitaifa na kimataifa; magenge yanayochochea utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kimaadili, kitamaduni na kiutu! Hii inatokana na ukweli kwamba, rushwa inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu! Rushwa ina tabia ya kujigeuza geuza kadiri ya mazingira na vionjo vya mtu, kumbe, hakuna anayeweza kujidai kwamba, rushwa ameipatia kisogo! Jambo la msingi ni kuwa macho na makini; kwa kukesha na kusali, ili kutokutumbukia majaribuni!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua katika utangulizi wa kitabu kuhusu “Rushwa” kwamba, ina tabia ya kutaka kutanuka na kujigamba; kusambaa na kuenea kwa haraka kama moto wa mabua! Ina tabia ya kujikweza na kujiona bora kuliko wengine, kiasi cha mtu kuweza kujenga dharau na tabia ya kutowajali wengine! Mdhambi anaweza kuwa na ujasiri wa kuomba msamaha, lakini mla rushwa na fisadi ni watu wenye moyo mgumu na ni vigumu sana kuomba msamaha. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina budi kusikiliza kwa makini na kuwa na ujasiri wa kunyanyuka na kuanza kuganga na kuponya madonda na majeraha ya ukosefu wa matumaini mintarafu huruma ya Mungu. Kanisa lifanye kazi hii kwanza kabisa kwa kujisafisha lenyewe, bila woga wala makunyanzi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, rushwa ndani ya Kanisa ni ile tabia ya wakleri, watawa na waamini kupenda na kumezwa mno na malimwengu; inajionesha katika utepetevu wa imani; tabia ya unafiki na watu kutaka umaarufu wa mpito, tamaa ya mali na madaraka. Kanisa linaweza kushinda kishawishi cha rushwa na ufisadi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kumjengea uwezo wa kutoka kifua mbele ili kulinda na kudumisha mambo msingi. Kanisa halina budi kujielekeza katika kusimamia na kutekeleza misingi ya haki , huruma na upendo; kwa kukazia kipaji cha ubunifu, umoja na mshikamano, ili kupyaisha maisha ya binadamu dhidi ya rushwa na ufisadi, sumu kali dhidi ya utu na heshima ya binadamu!

Rushwa ni mapambano yanayowashirikisha watu wote kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kukazia majiundo makini na endelevu yanayofumbatwa katika utamaduni wa huruma ya Mungu. Ni mapambano yanayohitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa watu wote wenye mapenzi mema, ili kutambua na hatimaye, kutibu na kuganga saratani ya rushwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.