2018-07-12 08:59:00

Siku ya Sala ya Kiekumene, mwanzo wa mapambazuko mapya ya umoja


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema, Viongozi wa Makanisa pamoja na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati, Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 wameungana kwa pamoja kuadhimisha Siku ya Sala ya Kiekumene ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. 

Hii ni hija ya uekumene wa sala na maisha unaowabidisha kufanya hija ya pamoja, inayofumbatwa katika ukarimu na nguvu ya maisha ya kiroho kiasi hata cha kujisikia kuwa karibu zaidi, kama ilivyokuwa Siku ya Kuombea Amani mjini Assisi; kwa kujikita katika udugu katika Kristo Yesu na kwa njia ya maombezi ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari anayeheshimiwa sana katika jitihada zake za kiekumene, viongozi hawa wakapata muda wa kusali na kutafakari kuhusu hatima ya Wakristo huko Mashariki ya kati. Imekuwa ni siku ya pekee kabisa ambayo Wakristo kutoka Mashariki na Magharibi wakaweza kukutana na kusali kwa pamoja mjini Bari, Kusini mwa Italia.

Ukanda wa Mashariki ya Kati katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni limegeuka kuwa ni uwanja wa fujo: vita, ghasia na uharibifu mkubwa wa zawadi ya maisha, mali za watu na miundo mbinu. Kumekuwepo na uvamizi na uporaji wa rasilimali asilia na kwamba, Ukanda wa Mashariki ya Kati sasa umekuwa ni chimbuko la misimamo mikali ya kidini na kiimani, uhamiaji wa shuruti pamoja na baadhi ya watu kutelekezwa. Kumekuwepo na kimya kikuu kwa watu wengi na baadhi yao kuhusika moja kwa moja.

Mashariki ya Kati limekuwa ni eneo ambalo watu wake wanalikimbia, kiasi cha kutishia uwepo wa imani ya Kikristo katika eneo hili, lakini, ikumbukwe kwamba, bila Wakristo utambulisho wa Mashariki ya Kati unaingia dosari kubwa. Kardinali Sandri anakaza kusema, katika unyenyekevu wote anaweza kusema, kwa hakika siku hii imekuwa na mafanikio makubwa, kwa kuliwezesha Kanisa kujielekeza zaidi katika Ukanda wa Mashariki ya kati, ili kutafakari, kusali na kuangalia: matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika eneo hili ambalo ni eneo asilia la Ukristo. Bila kusahau hata kidogo mateso, mahangaiko na matarajio ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kwa wakati huu wamependa kujielekeza zaidi huko Mashariki ya Kati kwa kuangalia madhara ya vita huko Siria na Iraq, hali ambayo imesababisha vifo, uharibifu mkubwa wa miundo mbinu pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi yao wenyewe. Bila Wakristo, utambulisho wa Mashariki ya Kati unapwaya sana anasema Kardinali Sandri.

Wakati wa mkutano wao wa faragha, sala, tafakari na chakula cha pamoja, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wameonesha moyo wa furaha na shukrani kwa Makanisa kuweza kukutana kwa ajili ya kutafakari na kusali, ili kuombea amani huko Mashariki ya Kati, wazo ambalo walilianzisha wao wenyewe na hatimaye, kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 7 Julai 2018. Viongozi wa Makanisa wamefurahishwa sana kwa: mapokezi, ukarimu na ushiriki mkamilifu  wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya kutafakari na kuombea amani huko Mashariki ya Kati. Wamefurahia sana umoja na mshikamano hata katika tofauti zao, ulioneshwa siku hiyo!

Viongozi wakuu wengine wa Makanisa waliwakilishwa vyema na kwa hakika imekuwa ni siku yenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wa Kanisa huko Mashariki ya Kati na hatua kubwa katika majadiliano ya uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa familia ya Mungu kama sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni ushuhuda wa umoja na mshikamano wa Kanisa, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Mababa wa Kanisa tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili wote wawe wamoja chini Kristo Mchungaji mkuu. Tazama inavyopendeza ndugu wakikaa kwa umoja na upendo!

Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa, Msimamizi wa Kitume wa Upatriaki wa Yerusalemu, mwanzoni mwa mkutano wao wa faragha alitoa hotuba elekezi na baadaye, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wakachangia mada kadiri ya Roho Mtakatifu alivyowawezesha. Wengi wamevutiwa sana na hotuba ya Askofu mkuu Pizzaballa kwa uchambuzi wake makini wa hali ya Mashariki ya Kati, wakachangia na kutoa maoni yao ya pamoja, msingi madhubuti wa utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa siku za usoni.

Mji wa Bari ulioko Kusini mwa Italia ni kitovu cha hija ya maisha ya kiroho kwa waamini wa dini na Makanisa mbali mbali. Ni mahali panapowaunganisha Wakristo kutoka Mashariki na Magharibi chini ya ulinzi na tunza ya maombezi ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari. Bikira Maria wa Odegitria, yaani Bikira Maria anayeonesha njia, anaheshimiwa sana huko Kusini mwa Italia kwa kuwa ni dira na mwongozo wa kumwendea Kristo Yesu, si tu kwa njia ya maneno, bali kwa ushuhuda wa maisha, yaani kwa njia ya uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii.

Hali ya Ukanda wa Mashariki ya Kati bado ni tete sana kutokana na vita, mauaji na uharibifu mkubwa unaofanywa kwenye miundo mbinu! Kuna mateso na mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu katika eneo hili. Ni matumaini ya viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kwamba, wahusika wakuu wa majanga na maafa makubwa yanayoendelea kujitokeza huko Mashariki ya Kati, wamesikia ujumbe kutoka Bari, basi wasutwe na dhamiri nyofu, tayari kusikiliza kilio cha familia ya Mungu inayotaka: haki, amani, uhuru na maridhiano kati ya watu kama kielelezo makini cha maendeleo endelevu na fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.