2018-07-10 15:30:00

Viongozi wa Kanisa washambuliwa nchini Nicaragua! Maaskofu washutumu!


Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Nicaragua limesikitishwa sana na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama dhidi ya Kardinali Leopoldo Brenes, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Managua, Nicaragua, Askofu msaidizi Josè Silvio Bàez pamoja na Askofu mkuu Waldermar Stanislaw Sommertag, Balozi wa Vatican nchini Nicaragua. Maaskari hao wamewashambulia viongozi wa Kanisa kwa vitendo na maneno makali na baadhi yao kuporwa vitu vya thamani, walipokuwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Sebastiano, huko Diriamba.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua linasema, viongozi hawa walikuwa wanawapelekea msaada wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Bartolomeo. Maaskofu wanalaani sana vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyofanywa na askari hawa, wakati ambapo viongozi wa Kanisa walikuwa wakitekeleza dhamana na wajibu wao wa kitume. Hii ilikuwa ni ziara ya kikazi kwa ajili ya kuwafariji wanaoteseka kutokana na dhuluma, nyanyaso na vipigo kutoka kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama nchini Nicaragua.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica, chini ya uongozi wa Askofu mkuu Josè Rafael Quiros Quiros, limeungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua kulaani vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyofanywa na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama. Maaskofu wanasema, inasikitisha kuona kwamba, Serikali iliyoko madarakani inawanyanyasa na kuwatendea vibaya wananchi wake wasiokuwa na hatia.

Maaskofu wa Costa Rica wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujihusisha kwa karibu zaidi na machafuko ya kisiasa nchini Nicaragua, ili kuweza kupata suluhu ya kudumu vinginevyo kuna hatari kwa nchi kutumbukia katika maafa makubwa. Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica linakimbilia ulinzi na tunza ya kimama ya Bikira Maria, Mkingiwa Dhambi ya Asili aweze kuwalinda na kuwasimamia watoto wake wanaoteseka huko nchini Nicaragua.

Naye Rais Daniel Ortega wa Nicaragua amesema, hana sababu msingi za kuitisha uchaguzi mkuu kwa wakati huu kama njia ya kudhibiti machafuko ya kisiasa nchini mwake. Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama inatoa: kanuni, sheria na taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa na Serikali  katika masuala ya uchaguzi mkuu. Hili ni ombi ambali lilikuwa limetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Nicaragua na kuungwa mkono pia na vyama vya upinzani nchini humo.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua ili kuonesha masikitiko yake kutokana na machafuko pamoja na ghasia zinazoendelea nchini humo, ambazo tayari zimepelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa vibaya. Kikundi cha watu wenye silaha kinachounga mkono serikali iliyoko madarakani kimeamua kuanzisha mashambulizi ya silaha ili kupambana na raia wanaopinga mchakato wa mageuzi unaofanywa na serikali ya Nicaragua.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na mashambulizi haya. Anasema, Kanisa daima litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano, yanayohitaji uwajibikaji unaomwilishwa katika matendo kwa kuheshimu uhuru wa watu, lakini zaidi kwa kuheshimu maisha ya watu! Baba Mtakatifu anaiombea nchi ya Nicaragua, ili iweze kusitisha ghasia na hatimaye, kuwa na uhakika wa kuanza tena majadiliano katika ukweli na uwazi!

Tangu tarehe 18 Aprili 2018 kumekuwepo na maandamano makubwa ya kupinga mchakato wa mageuzi ya masuala ya pensheni kwa kupunguza kiasi cha asilimia 5%, mchakato ambao ulikuwa umeridhiwa na Rais Daniel Ortega wa Nicaragua. Baada ya mshike mshike na patashika nguo kuchanika, Rais Daniel Ortega, akanyoosha mikono juu na kuondoa muswada wa mageuzi! Lakini, wananchi wakaendeleza mapambano kwani walisema, Rais Daniel Ortega, ndiye aliyekuwa “mzigo kwa Serikali” baada ya kuongoza Nicaragua kwa muda wa miaka 30.

Wachunguzi wa mambo wanasema, hadi sasa kuna watu zaidi 100 wamefariki dunia baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kuwarushia risasi za moto wananchi waliokuwa wanaandamana kudai haki zao pamoja na kumtaka Rais Daniel Ortega, kung’atuka kutoka madarakani haraka iwezekanavyo! Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu, likaamua kuingilia kati ili kuanzisha mchakato wa majadiliano kati ya Serikali na raia wake, ombi lililokuwa limetolewa na Rais Daniel Ortega. Lakini kwa sasa, Rais Ortega amefutilia mbali mchakato wa majadiliano na kwamba, kwa sasa ameamua kuwashughulikia wananchi wake kama “Mbwa koko”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua katika tamko lake, linasikitika na kulaani mashambulizi dhidi ya raia na kwamba, hivi ni vitendo vinavyokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Maaskofu wanakaza kusema, raia wanao uhuru wa kuandamana kikatiba, lakini Serikali imeamua kuwashughulikia bila huruma, kiasi hata cha kuwafutilia mbali kutoka katika uso wa dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.