2018-07-09 15:21:00

Siku ya Mabaharia Duniani kwa Mwaka 2018


Bwana Kitack Lim Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Shughuli za Majini,  IMO, katika ujumbe wake kwa Siku ya Mabaharia Duniani kwa Mwaka 2018 iliyoadhimishwa tarehe 25 Juni, anasema, usafirishaji bora na wenye tija baharini hutegemea sana ustawi wa mabaharia.  Ni katika muktadha huo, shirika hilo linaendelea kuhamasisha jumuiya ya Kimataifa katika kuweka  kwenye mazingira bora ya ustawi na afya ya mabaharia ili kuwaepusha na matatizo ya kiafya ikiwemo msongo wa mawazo. Mabaharia hufanya kazi ngumu sana ambayo inahitaji kuwa makini kiafya na kiakili. Usalama wa kazi ya majini  unategemeana na utaalamu na majitoleo ya  mabaharia, licha ya maendeleo makubwa ya kisasa katika teknolojia. Kazi zao zinaweza kuwa na manufaa katika kujipatia kipato ila wakati mwingine ina changamoto nyingi huko baharini ikiwa ni pamoja na likizo fupi,  kuachishwa kazi, migogoro ya malipo ya mishahara na pia walengwa katika uharamia na ghasia za kutumia nguvu!

Anasema, jitihada za Shirika lake zitatimizwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya usalama baharini, ufanisi katika kuzuia na kudhibiti uharibifu wa mazingira utokanao na meli, pamoja na kuzingatia sheria za kimataifa zinazohusiana na ulinzi wa bahari chini ya mkataba wa IMO. Asilimia 80 ya biashara duniani hutegemea usafirishaji wa majini kupitia meli na hivyo, ustawi wa mabaharia ni ustawi wa mbinu hii ya usafirishaji ambayo siyo tu ni ya gharama nafuu bali pia ni njia inayotegemewa na watu wengi zaidi duniani. Siku ya kimataifa ya Mabaharia Duniani, huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Juni, ambapo mwaka huu kaulimbiu ni kuchagiza ustawi wa mabaharia kimwili na kiakili. Itakumbukwa kwamba, Shirika la Kimataifa la Shughuli za Majini, IMO, mwaka 2018 linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni Shirika la Kimataifa linalojielekeza zaidi katika shughuli za bahari, usalama baharini, usafirishaji mizigo kimataifa pamoja na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira baharini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.