2018-07-05 16:51:00

Mkesha wa Sala ya Kiekumene kuombea amani na umoja Mashariki ya Kati


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati, tarehe 7 Julai 2018 wanaungana pamoja katika Siku ya Sala ya Kiekumene huko Bari, Kusini mwa Italia, kwa ajili ya kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”.   Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limechukua dhamana ya kuandaa mkesha wa tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuomba amani na urafiki kutoka kwa Mtakatifu Nicholaus wa Bari, kwa ajili ya Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika huko Mashariki ya Kati.  Mkesha huu utapambwa kwa Neno la Mungu, Sala na Tafakari kutoka katika hotuba mbali mbali za Baba Mtakatifu Francisko kuhusu amani kama zawadi ya Kristo Mfufuka kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anasema, leo hii watu wengi wana kiu ya haki, amani na utulivu wa ndani. Bado kuna watu wanaoteseka kutokana na vita, majanga asilia, umaskini na magonjwa. Biashara haramu ya silaha duniani, inaendelea kubomoa furaha ya maisha kwa kupandikiza utamaduni wa kifo; uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka! Kumbe, kuna umuhimu kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujibidisha kutafuta na kudumisha amani, utu na heshima ya binadamu!

Amani maana yake ni msamaha, toba na wongofu wa ndani. Ni matunda ya sala na mshikamano na Mwenyezi Mungu anayetaka kuganga na kuponyesha madonda ya ndani. Amani maana yake ni ukarimu, utayari, uwajibikaji na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Amani inajikita katika umoja, ushirikiano na mshikamano wa dhati, kwa kuthaminiana na kuheshimiana kama ndugu, ili kuitengeneza dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Amani ni elimu inayofumbatwa katika sanaa ya umoja, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana, kwa kutakasa dhamiri dhidi ya mambo yanayokwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu; utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Amani iwawezeshe watu kujenga na kudumisha: umoja, udugu na familia katika ngazi mbali mbali za maisha, ili kuvunjilia mbali: vita, chuki na uhasama, ili watu wote waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya familia ya Mungu inayowajibika na kutaabikiana! Pale ambapo mwanadamu anakosa majibu muafaka kwa changamoto mbali mbali anazokabiliana nazo katika maisha, majibu yanaweza kupatikana kwenye Fumbo la Msalaba, chemchemi ya huruma na upendo; msamaha na upatanisho; majadiliano, haki na amani. Ikumbukwe kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu! Kanisa linasali kwa ajili upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Sehemu ya pili ni ushuhuda kutoka katika Nyaraka za Mtakatifu Nicholaus hasa katika mchakato wa kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza maskini, yatima na wajane. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Nicholaus alikuwa na upendo na huruma kwa wale wote waliokuwa wananyanyaswa na kudhulumiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.