2018-07-04 14:55:00

Yaliyojiri katika ziara ya Kardinali Parolin nchini Montenegro & Serbia


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameipongeza Serikali ya Montenegro kwa kupiga hatua kubwa katika mchakato wa kutaka kujiunga na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na kukazia kwamba, hii ni Jumuiya inaosimikwa katika sheria kanuni na tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu! Amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kukuza na kudumisha: umoja na mshikamano wa kitaifa; udugu, haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Montenegro. Akiwa nchini Montenegro, amepata nafasi pia ya kutembelea Jumba la Makumbusho ya Mfalme Nikola, ili kujitajirisha na historia na umuhimu wa nchi hii kama mahali pa mkusanyiko wa watu, tamaduni na dini mbali mbali!

Kardinali Parolin, kuanzia tarehe 27-29 Juni 2018 amekuwa na safari ya kikazi nchini Montenegro pamoja na kujionea shughuli mbali mbali zinazofanywa na watawa pamoja na Kanisa katika ujumla wake kwenye sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii! Akiwa kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Shauri Jema, Tuzi, huko Montenegro, Kardinali Parolin, amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa na waamini walei kutoka Jimbo kuu la Bar Rrok Gjonlleshaj, kwa kuwataka kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuendelea kuchuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na udugu kama ulivyoshuhudiwa na Mitume mbali mbali waliyosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, Kardinali Parolin amewataka waamini kujichimbia katika mchakato wa kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha, kama unavyodadavuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume: “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12). Anakazia kuhusu mwaliko wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Kristo Yesu anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu kila mtu kadiri ya hali na wito wake; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Utakatifu kama anavyosema Papa Francisko ni chemchemi ya furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Utakatifu ni hija ya mapambano dhidi ya dhambi kwa kuendelea kupyaisha ile neema ya utakaso ambayo waamini wameipokea katika Sakramenti ya Ubatizo! Utakatifu unawawezesha waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wanaitwa kuwa watakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na ni kiini na utimilifu wa utakatifu wenyewe. Utakatifu ni changamoto inayopaswa kupaliliwa kila kukicha na kamwe haitoshi kuwa Mkristo na mwamini kuanza kubweteka, bali daima ajitahidi kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kardinali Pietro Parolin amemkumbuka kwa namna ya pekee Mtakatifu Leopoldo Mandic’, Mzaliwa wa Jimbo hilo, aliyejipambanua kwa kujisadaka. Mtakatifu Leopoldo Mandic’, alikuwa ni Padre aliyejua kuwatuliza na kuwafariji waungamaji: kwa maneno, ishara za upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, akawa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa waja wake. Mtakatifu Leopoldo alipenda kuwahakikishia waungamaji kuwa hata yeye alikuwa mdhambi kama wao, hivyo wasihofu, bali wawe na imani na kujiaminisha kwa Mungu mwenye huruma na upendo usiokuwa na kifani!

Kardinali Pietro Parolin, tarehe 30 Juni hadi tarehe Mosi Julai 2018 ametembelea nchini Serbia na huko akabahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa pamoja na Serikali. Amekazia kuhusu uhusiano mwema wa kidiplomasia kati ya Vatican na Serbia pamoja na kuonesha nia ya kutaka kuboresha mahusiano haya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya nchi hizi mbili. Amepongeza umoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Kanisa na kwamba, kila upande unapaswa kutekeleza wajibu wake, bila kuingiliana! Licha ya Kanisa Katoliki kuwa na waamini wachache nchini humo, lakini limekuwa na mchango mkubwa sana katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Ameitaka familia ya Mungu nchini Serbia kuendeleza majadiliano ya kiekumene na kidini. Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa imani inayomwilishwa katika kanuni maadili na utu wema, baada ya mwamini kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Amewapatia salam na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayetamani kuwatembelea, ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo.

Kardinali Parolin, akiwa nchini Serbia amezindua Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kimataifa la Watakatifu Cyril na Methodi. Haya Makao makuu ni sehemu muhimu sana ya kazi kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ni mahali pa huduma kwa Wakristo na kituo cha kuwakutanisha waamini wa dini mbali mbali pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Kardinali Parolin amehitimisha safari yake ya kikazi nchini Montenegro na Serbia kwa kusema kwamba kwa hakika imekuwa ni safari ya kihistoria, kwani imemwezesha kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuwatia shime waamini wa Kanisa Katoliki kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.