2018-07-04 14:33:00

Papa Francisko anakazia: Uekumene wa maisha, damu na utakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati, tarehe 7 Julai 2018 wanaungana pamoja katika Siku ya Sala ya Kiekumene huko Bari, Kusini mwa Italia, kwa ajili ya kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. Mji wa Bari unahifadhi masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari, kiungo muhimu sana katika majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa ya Mashariki.

Hii ni siku ambayo inapambwa kwa mambo msingi katika uekumene wa sala yaani: Sala ya kiekumene ufukweni mwa Bahari; tafakari na kusikilizana kati ya Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo. Haya yamesemwa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumanne, tarehe 3 Julai 2018, kuhusu Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Mashariki ya Kati. Hii ni siku maalum kwa ajili ya kuombea amani na umoja wa Makanisa.

Baba Mtakatifu Francisko amekazia mambo makuu matatu katika kudumisha majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Mashariki: Uekumene wa sala ambao amekuwa akiutekeleza mara kwa mara anapokutana na viongozi wakuu wa Makanisa wanapokutana. Amekazia pia uekumene wa damu unaoshuhudiwa na Wakristo kutoka Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu ameendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini kama njia ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kama ilivyojitokeza kwa Siku ya Sala na Kufunga kwa ajili ya Siria, iliyoadhimishwa mwezi Septemba 2013.

Kumbe wazo la kusali kwa ajili ya kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati linapata chimbuko lake kutoka kwa viongozi wa Makanisa na kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko kama ushuhuda wa uekumene wa sala. Kardinali Bèchara Boutros Rai, kwa niaba ya viongozi wa Makanisa ya Mashariki, walimwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko kumwomba kuwa na siku maalumu ya sala kwa ajili ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Maandalizi ya siku hii yamevihusisha vyombo vya ulinzi na usalama, Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pamoja na Jimbo kuu la Bari-Bitondo, lililoko Kusini mwa Italia.

Kwa upande wake Kardinali  Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza viongozi wa Makanisa katika tukio hili maalumu, kwa kukumbuka kwamba, Mashariki ya Kati ni kiini cha Ukristo. Siku hii inapania kukuza na kudumisha majadiliano ya upendo na amani kama ilivyojitokeza kunako mwaka 1964, Mwenyeheri Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Athenagora wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaolenga kwa namna ya pekee kabisa umoja wa Wakristo. Idadi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati inaendelea kupukutika kila kukicha na kwamba, kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Idadi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati ilikuwa ni sawa na 40%, leo hii, idadi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati ni asilimia 4%.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa maisha unaofumbatwa katika uekumene wa damu na hatimaye, uekumene wa utakatifu wa maisha. Haya mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo huko Mashariki ya Kati, katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.

Uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Kanisa linapenda kuona kwamba, Wakristo wanabaki katika eneo lao la asili. Utambulisho wa Mashariki ya Kati unafumbatwa kwa uwepo endelevu na ushuhuda wa Wakristo na kwamba, makundi ya waamini wachache ndani ya jamii yanapaswa kulindwa na kwamba, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini katika ukweli, uwazi na upendo. Lengo ni kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.