2018-07-04 06:50:00

Mafundisho Jamii ya Kanisa yasaidie kuyatakatifuza malimwengu!


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, yanaongozwa na kauli mbiu “Sera na mtindo mpya wa maisha katika kipindi cha digitali”. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, alitamani sana kuona kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapata hekima inayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuboresha sera na mikakati ya kiuchumi, biashara na huduma za kijamii. Hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa katika jukwaa la Jumuiya ya Kimataifa ambamo kuna changamoto changamani zinazoingiliana.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kama sehemu ya maadhimisho haya amesema, changamoto kubwa inayoendelea kuathiri mfumo mzima wa uchumi ni kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema na matokeo yake ni kushamiri kwa ubinafsi na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; hali inayoathiri utu na heshima ya familia ya binadamu. Ushirikiano wa karibu na wadau katika sekta ya uchumi na fedha, viongozi wa vyama na mashirikisho ya wafanyakazi pamoja na wafanyakazi wa umma ni muhimu sana ili kuweza kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika medani mbali mbali za maisha!

Ni katika mapambazuko ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, familia ya Mungu Afrika ya Kusini nayo Alhamisi, 31 Mei 2018 imeanzisha Jukwaa la Wafanyabiashara Wakatoliki, ili kuwasaidia waamini kuimarisha imani yao kwa kuiadhimisha na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wao kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Hili ni jukwaa linalopania kujikita katika: sheria, kanuni maadili; nidhamu, weledi, uadilifu, uwajibikaji na huduma katika jamii. Jukwaa pia linapania kukuza na kuimarisha mahusiano na mafungamano miongoni mwa wafanya biashara wakatoliki, ili kusaidiana katika kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika maisha na utume wao.

Pole pole, Jukwaa hili litaweza kutanua matamvua yake hadi kuwafikia wanataaluma na wafanyakazi wa umma ndani na nje ya Afrika ya Kusini. Waasisi wa Jukwaa hili wanasema, umefika wakati kwa waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na wajibu unaowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kwa hakika Jukwaa la Wafanyabiashara Wakatoliki linapaswa kuwa ni sauti ya Kanisa katika masuala ya biashara, kanuni maadili na utu wema!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kuna mpasuko mkubwa kati ya sayansi na imani, kiasi kwamba, kanuni maadili na utu wema, havina nafasi tena katika masuala ya uchumi na fedha. Matokeo yake ni watu kutafuta faida kubwa zaidi bila ya uwajibikaji wa kijamii. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya kiuchumi inajikita katika kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha ya kijamii na wala si mambo yanayotoka nje. Hili ni lengo la muda mrefu linalopaswa kufanyiwa kazi kwa kuwashirikisha watu binafsi na taasisi mbali mbali katika “tumbo” la maisha ya kijamii. Mchango wa Mafundisho Jamii ya Kanisa hauna budi kuwajengea vijana na familia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kujenga utamaduni wa utandawazi wa haki uchumi, usawa na ushirikishwaji wa watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.