2018-07-03 08:44:00

Waraka wa Mwenyeheri Paulo VI kwa Mapadre Duniani


Miaka 50 imegota, tangu Mwenyeheri Paulo VI alipowaandikia wakleri Waraka maalumu, kama sehemu ya kufunga Mwaka wa Imani, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya karne ya 19 tangu Watakatifu Petro na Paulo, walipoyamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa. Hii ilikuwa ni tarehe 30 Juni 1968, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha kumbu kumbu ya Mashahidi wa Roma, waamini waliosadaka maisha yao kwa ajili ya ushuhuda wenye nguvu kwa Kristo na Kanisa lake, na damu yao ikawa ni mbegu ya Ukristo, sehemu mbali mbali za dunia!

Itakumbukwa kwamba, ni katika Wosia wake wa Kitume “Petrum et Paulum apostolos” yaani “Mitume Petro na Paulo” ulioandikwa mwaka 1967 ulioanzisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, Miamba wa Kanisa inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Haya yalikuwa ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Mababa wa Kanisa wakataka Mitume hawa waliotangaza na kushuhudia imani yao kwa njia ya maisha yao, wakumbukwe na Kanisa zima!

Mwenyeheri Paulo VI anakaza kusema, hii ni “Kanuni ya Imani ya Watu wa Mungu” iliyotangazwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanarejea tena na tena kwenye chemchemi ya imani na mafundisho ya Kanisa. Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake kwa Wakleri, anawakumbusha kwamba, wao kwanza kabisa ni wachungaji wa Kondoo wa Kristo. Anatambua fika: jitihada zao katika kutangaza Neno la Mungu, kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na kuwahudumia watu wa Mungu katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili.

Kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, Mwenyeheri Paulo VI anasema, anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na Wakleri wote, waliokabidhiwa dhamana na utume wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hii ni changamoto ya kuendelea kutoa ushuhuda wenye mvuto katika maisha na utume wa Kanisa. Wito, maisha na utume wa Kipadre upewe kipaumbele cha kwanza. Huu ni wosia wa kibaba unaotolewa kwa moyo mnyofu, katika ukweli na uwazi na kwamba, hii ni changamoto kwa Wakleri kuweza kuupokea wosia huu na kuufanyia kazi katika maisha na utume wao!

Waamini wanathamini maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu na hatimaye, kumwilishwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Neno la Mungu linafafanua na kukazia zaidi kwamba, Mwenyezi Mungu anafahamu fika mambo yao yote, anajua bidii yao, uvumilivu kwa watu waovu na watenda dhambi na kwamba, wamewapima wale wanaojidai kuwa mitume na kumbe si mali kitu!

Mwenyeheri Paulo VI anawashukuru na kuwapongeza wakleri wenye saburi, wenye uwezo wa kuvumilia taabu na mateso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake pasi na kuvunjika moyo! Lakini, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Wakleri wanapyaisha kila siku ya maisha yao ule upendo waliokuwa nao siku ile ya kwanza, walipoitwa na kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao! Wakleri watambue kwamba, wao ni watumishi wa Kristo, waliokabidhiwa siri za Mungu na kwamba, wanatakiwa kuwa waaminifu na watu wenye dhamiri nyofu bila mawaa mbele ya Mungu na jirani zao.

Wakleri ni waalimu wa mambo matakatifu, wagawaji wa mafumbo ya Mungu na marafiki wa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu. Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, wasaidiane, wataabikiane na kushikamana, ili kuweza kuyapatia matatizo na changamoto hizi ufumbuzi wa kudumu katika mwanga wa Injili. Mwenyeheri Paulo VI anasema, alitaka kuwashirikisha haya mambo mazito yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake, ili wakleri watambue kwamba, Kanisa linawathamini na kujali mchango wao katika mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Mapadre wajitahidi kadiri wanavyoweza kuwa na umoja na mshikamano kamili na Maaskofu wao, ili kuweza kupata amani, utulivu wa ndani na furaha ya kutangaza na kushudia Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.

Mwenyeheri Paulo VI anatambua fika: matatizo na changamoto zinazowakabili Wakleri sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, hawaoni tena ile furaha ya maisha na wito wa kipadre, kiasi hata cha kujiachilia na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Mapadre wakumbuke kwamba, mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika duniani, hayatawaacha salama, ikiwa kama hawatakuwa imara katika imani, maadili na utu wema! Itakuwa ni vigumu sana kwa watu wasiokuwa na imani, kuelewa ubinadamu na udhaifu wa Mapadre katika maisha na utume wao! Kumbe, hii ni changamoto kwa wakleri kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kufa na kupona kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake; watu wenye mvuto na mashiko; watu wasiokuwa ni kikwazo cha imani kwa wale wanaowaona na kukutana nao katika safari ya maisha yao!

Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, Mapadre, wasipate kishawishi cha hofu kuhusu maisha na wito wao, bali watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Daraja takatifu, wanashiriki Ukuhani wa Kristo! Kumbe, wao kimsingi ni watu wa Mungu na watumishi wa Kristo Yesu na Kanisa lake! Wao wanatenda kwa niaba ya Kristo “Agunt in persona Christi” kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivyo wanakuwa ni madaraja kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya huduma ya Mafumbo ya Kanisa! Wakleri ni watu wanaoishi si kwa ajili yao binafsi, bali kwa ajili ya jirani zao, lakini zaidi kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Katika changamoto za maisha, kashfa na udhaifu wa kibinadamu unaoshuhudiwa na Wakleri sehemu mbali mbali za dunia, watu wanajiuliza, Je, bado kuna sababu ya kuwa na Mapadre ndani ya Kanisa? Mwenyeheri Paulo VI anadadavua kwa kusema, katika Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, bado kuna kiu na hitaji kubwa la Mapadre wema, watakatifu na waadilifu; watu watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Kweli za Kiinjili kati ya watu wa Mataifa! Watu wana kiu ya: Imani, matumaini na mapendo; wanataka kuonja huruma na msamaha wa Mungu katika maisha yao! Watu wa Mungu wanataka kuwaona Mapadre wanaojichanganya kwa ajili ya malezi na utume kwa vijana wa kizazi kipya; Wakleri watakaosaidia kufundisha dini, maadili na utu wema shuleni; Mapadre watakaochakarika kila siku kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na wazee!

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu anakaza kusema Mwenyeheri Paulo VI na kwamba, ulimwengu unalihitaji Kanisa na wala hakuna Kanisa lisilokuwa na wahudumu walioandaliwa vyema, wakawekwa wakfu kama alama ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake na kutumwa kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wa Mataifa. Wao ni vyombo na mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake, lakini wanapaswa kutambua kwamba, wito na maisha yao yamehifadhiwa katika vyombo vya udongo! “Habemus...thesaurum istum in vasis fictibus, ut sublimitas sit virtutis Dei et non ex nobis” (Rej. 2 Kor. 4:7).

Tiba ya magonjwa ya kiroho katika maisha na utume wa Mapadre ni: Sala ya Kanisa ndio msingi wa majadiliano ya maisha ya kiroho kati ya Mapadre na Mwenyezi Mungu, ni nguvu ya maisha ya ndani inayojenga na kuimarisha utashi na dhamiri nyofu. Ni mwaliko wa kukuza na kudumisha usafi kamili kama sadaka na utimilifu wa upendo na huduma kwa Mungu, Kanisa sanjari na mpango wa Mungu wa wokovu kwa ulimwengu. Mapadre wakuze na kudumisha umoja, udugu, upendo na mshikamano katika maisha ya kijumuiya, kwani wanaitwa na kutumwa kama Jumuiya na wala si kama mtu binafsi!

Mapadre ni sehemu ya Jimbo na Kanisa la Kiulimwengu, changamoto na mwaliko wa kuwa na imani kwa Kristo na Kanisa lake. Watambue kwamba, Kanisa linaundwa na wadhambi wanaojibidisha kwa toba na wongofu wa ndani ili kuweza kupyaisha maisha yao! Kanisa linaundwa na watakatifu, wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu na kwa neema ya Mungu leo hii wamekuwa kama walivyo! Mapadre walipende Kanisa katika utakatifu na udhaifu wake; washiriki kikamilifu katika mchakato wa utakatifu, ili kuboresha ile sura ya Kanisa ambalo ni Mchumba wa Kristo!

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu inayoongozwa na Roho Mtakatifu inayohitaji umoja na ushirikiano wa watoto wake wote! Waamini wote wawe na ujasiri wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kupyaisha maisha yao kwa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa mwanga wa Injili. Waendelee kujikita katika mchakato wa mageuzi ya Kiliturujia na kwamba, Kanisa liwe ni chombo makini cha huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa liendelee kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Liwe ni chombo cha amani na maridhiano kati ya watu kwa kujikita katika majadiliano ya kiekumene na kidini; ili kudumisha uhuru wa kidini, nguzo msingi ya haki za binadamu. Mapadre wakuze na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa, ili aweze kuwafariji na kuwategemeza kwa ulinzi na tunza yake ya kimama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.