2018-07-03 15:43:00

Mh. Padre Bermiro Cuica Chissengueti ateuliwa kuwa Askofu wa Cabinda


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Belmiro Cuica Chissengueti, C.S.Sp., wa Shirika la Roho Mtakatifu, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Cabinda, nchini Angola. Kabla ya uteuzi wake, Askofu mteule Belmiro Cuica Chissengueti, C.S.Sp., alikuwa ni Padre mkuu wa Kanda, Shirika la Roho Mtakatifu nchini Angola. Alizaliwa tarehe 5 Machi 1969. Baada ya masomo na majiundo yake kitawa akaweka nadhiri za daima hapo tarehe 5 Agosti 1995 na hatimaye tarehe 5 Mei 1996 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Baadaye alitumwa na Shirika lake kujiendeleza kwa masomo ya juu kuhusu Sheria za Nchi katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Angola na hatimaye kujipatia shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Pablo de Olavid kilichoko nchini Hispania. Kwa miaka kadhaa alifanya mazoezi kwenye Chama cha Mawakili wa Angola na huko akajipatia uzoefu wa kutosha katika masuala ya Sheria za Nchi.

Baada ya Upadrisho wake, Askofu mteule Belmiro Cuica Chissengueti, C.S.Sp., amewahi kuwa Paroko usu; mjumbe mshauri wa Kanda ya Shirika la Roho Mtakatifu nchini Angola; Paroko na baadaye akateuliwa kuwa Makamu Askofu Jimbo kuu la Luanda na Mjumbe wa Halmashauri ya Mapadre Jimbo kuu la Luanda, Angola. Tangu mwaka 2004 hadi mwaka 2013 alichaguliwa kuwa mshauri wa kanza wa Kanda ya Mapadre wa Roho Mtakatifu nchini Angola. Tangu mwaka 2010 hadi mwaka 2014 akateuliwa kuwa ni Katibu mkuu, Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe. Mwaka 2016 akateuliwa kuwa Padre Mkuu wa Kanda, Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu nchini Angola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.