2018-06-30 08:05:00

Dhamana na wajibu wa Makardinali katika maisha na utume wa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 28 Juni 2018 amewatunukia heshima Makardinali wapya 14 na kuwakumbusha kwamba, Kristo Yesu alipokua anatangaza kuhusu Fumbo la Pasaka, aliwaambia kwamba, anawatangulia na mtu yoyote anayetaka kuwa mkubwa kati yao, anapaswa kuwa mtumishi wao! Ujumbe huu ni matokeo ya malumbano yaliyojitokeza miongoni mwa Mitume wa Yesu, waliokuwa wanatafuta nafasi za kwanza; wengine wakaelemewa na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kipaumbele cha kwanza kinatolewa kwa ajili ya utume wa Kanisa! Malumbano kama haya anasema Baba Mtakatifu si ajabu yakajitokeza hata kwenye nafasi mbali mbali za uongozi ndani ya Kanisa.

Patriaki Louis Raphael Sako, kwa niaba ya Makardinali wapya, alitoa shukrani za dhati kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwaamini na kuwateua kuwa ni washauri wake wa karibu, kielelezo makini kinachoonesha ukatoliki wa Kanisa, kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu duniani! Waamini wa dini mbali mbali, wameonesha moyo wa shukrani kwa uwazi wa Kanisa Katoliki katika maisha na utume wake na kwa namna ya pekee kabisa kwa uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Waamini wa dini mbali mbali wanasema, Papa Francisko ni kiongozi ambaye ameguswa na mahangaiko, mateso, hofu, mashaka na matamanio halali ya watu wa Mungu, lakini kwa namna ya pekee kabisa kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, Pakistani na maeneo ambayo yanakabiliwa na vita pamoja na machafuko ya kidini; ambayo yamekuwa ni chemchemi ya  mashuhuda wa Injili ya Kristo na Kanisa lake huko Mashariki ya Kati. Makardinali wapya wanasema wanaendelea kumwombea Baba Mtakatifu ili juhudi zake ziweze kuleta toba na wongofu wa ndani; haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi.

Uteuzi wa Makardinali wapya ni changamoto kubwa inayowataka kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima wakijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Makardinali wanaojitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili. Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu.

Jicho la kibaba linalooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, ni chachu ya matumaini na mapendo ambayo yanapaswa kutawala katika maisha ya watu! Ni matumaini ya Makardinali wapya kwamba, baada ya vita na mateso kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, hatimaye, siku moja, amani na utulivu vitaweza kutawala katika akili na nyoyo za watu! Damu ya mashuhuda wa imani sehemu mbali mbali za dunia, kwa hakika ni mbegu ya Ukristo itakayozaa matunda kwa wakati wake! Makardinali wanasema, wataendelea “kujichimbia” katika mchakato wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kudumisha sanaa ya majadiliano; wataendelea kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; tayari kupambana na changamoto mamboleo na kuzitafutia ufumbuzi wake kwa mwanga wa Injili na imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Makardinali wapya wamerudia tena uaminifu, upendo na majitoleo yao kwa Kristo na Kanisa lake, bila kuisahau familia ya Mungu wanayopaswa kuihudimia. Wanataka kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya furaha; imani, upendo, sadaka, huruma na msamaha. Wanataka kuwa kweli ni madaraja na wajenzi wa misingi ya haki na amani, ili kufutilia mbali utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; ulimwengu ambao kwa sasa unaelemewa na ulaji wa kupindukia; uchu wa mali na madaraka!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake alikaza kusema, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kujikita katika toba na wongofu wa ndani; mabadiliko ya maisha ya kiroho na mageuzi ya Kanisa mintarafu mwanga wa umisionari, ili kuondokana na tamaa ya mambo binafsi, tayari kuanza kuangalia, ili hatimaye, kuanza kujikita katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha. Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuondokana na dhambi pamoja na ubinafsi, ili kujikita katika uaminifu na uwajibikaji, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kanisa.

Mara baada ya Liturujia ya kuwasimika Makardinali wapya, wakiwa wameandamana na Baba Mtakatifu Francisko, kwa pamoja walipanda Bus kuelekea kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” anakoishi Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ili kumsalimia na kumtakia heri kwa ajili ya Sherehe ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume. Makardinali wapya, walibahatika kupewa baraka ya kitume kutoka kwa Papa Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, kurejea kuendelea na shughuli zilizopangwa kwa siku hiyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.