2018-06-29 11:12:00

Utukufu wa Mungu na ukuu wa binadamu katika kazi ya uumbaji!


Mwenyezi Mungu ameuumba ulimwengu katika ukamilifu wake na kwa namna ya pekee amempatia mwanadamu cheo kikubwa kuliko viumbe vyote kwa kumfanya kwa mfano wa sura yake (Rej Mw 1:26ff). Mzaburi anajiuliza juu ya upendeleo aliopewa na Mungu akisema: “Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako… mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima” (Zab 8:3 – 4). Hivyo tangu mwanzo mwanadamu hakuumbwa katika uovu au ukosefu wa namna fulani. Ameumbwa katika ukamilifu wote na kupewa utukufu na heshima ya kipekee. Mwanadamu ameinuliwa sana na kupewa hadhi ya kutawala na kuratibu kazi yote ya uumbaji. Katika ukweli huu tunapatwa na mkanganyiko pale tunapoona mambo mabaya yamemwelemea mwanadamu.

Je, mambo haya mabaya yametokea wapi? Je, chanzo chake kinaweza kuwa ni Mungu? Wanafalsafa na wanataalimungu maadili wanaelezea jambo lolote baya kama ukosefu wa ukamilifu. Kwa maneno mengine ni ukosefu wa uhalisia wa kitu. Hivyo mambo mabaya husababisha upungufu na matokeo yake ni utendaji hafifu au kukosekana kwa utendaji uliokusudiwa. Ubaya ni hitilafu inayoingia katika mfumo au mtindo fulani wa maisha. Kiroho ubaya huonekana kama uovu na unaelezewa kwa neno “dhambi”. Hii ni namna ambayo inamkuta mwanadamu anapokosa utii kwa amri na maagizo ya Mungu, matokeo ya uasi kwa Mungu. Mwanadamu aliyeumbwa kikamilifu kiroho, kimwili na kiakili anaingia katika uovu pale anapokosa hali fulani ya ukamilifu kadiri ya uumbaji na matokeo yake huwa ni ugonjwa, mahangaiko, mifadhaiko ama kuingia katika hali ya mauti kimwili au kiroho.

Masomo ya dominika ya leo yanatutafakarisha juu ya chanzo cha uovu ambao ni huzuni kwa mwanadamu na mwarobaini wake unakuja kwa njia ya Yesu Kristo. Somo la kwanza linatuonesha chanzo cha uovu. Mauti si mpango wa Mungu bali imemuingia mwanadamu sababu ya wivu wa ibilisi. Mwandishi wa kitabu cha Hekima anaweka wazi kabisa kwamba Mungu amemuumba mwanadamu kwa maisha ya umilele na kutokuharibika, yaani kushiriki pamoja na Mungu katika heri ya milele. Yeye ameviumba vitu vyote vizuri (Rej Mw 1:31). Mwanadamu ameumbwa katika utakatifu. Tangu uumbaji mwanadamu amekirimiwa tunu hii ya kimungu. Hivyo kubaki mwaminifu kwa Mungu ndiyo ilikuwa kibali kwake katika kuutunza utakatifu wake.

Kifo kinacholetwa na dhambi si kifo cha kimwili bali ni ule utengano kati ya mwanadamu na Mungu sababu ya hukumu ya dhambi. Kwa maneno mengine, mwanadamu anapokuwa bila Mungu anakuwa katika hali ya ukosefu na kupungukiwa. Dhambi ya asili inalifafanua wazi jambo hili. Mwanadamu alikengeuka na kutaka kutenda mambo bila Mungu ili kujitwalia nafasi ya Mungu maishani mwake. Ni hali ambayo inaendelea kuonekana hata leo katika jamii ya “kisekulari” ambayo inafanya bidii ya kuigawa dini na maisha ya kawaida ya mwanadamu. Matokeo yake yanashuhudiwa kila uchwao kwa anguko kubwa la mwanadamu. Vita, magonjwa, malumbano, unyonyaji na mengineyo mengi ni matunda ya juhudi hizo za kibinadamu za kumwondoa Mwenyezi Mungu na katika maisha ya kila siku. Uovu unaomtafuna mwanadamu unaletwa na mwanadamu mwenyewe.

Injili inatuwekea mbele yetu Kristo kama mwarobaini wa msiba huu mkubwa unaomwandama mwanadamu. Matukio mawili ya uponyaji na uuhishaji ambayo yanarudisha furaha katika jamii ya mwanadamu yanatawaliwa na tunu ya imani. Imani thabiti kwa utendaji wa Mungu ndiyo uliomsukuma aliyeteseka kwa muda mrefu kujongea kwa Kristo kwa ujasiri, bila kujali umati wa watu au hali yake au namna alivyopokeleka sababu ya hali yake na matokeo yake anapona msiba wake: “Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule”. Hali kadhalikwa kwa mkuu wa sinagogi; bila kujali nafasi yake katika jamii katika masuala ya kidini anaitambua nguvu ya Mungu inayotenda ndani ya Kristo na kwa imani anaomba uponyaji kwa binti yake.

Kristo alimwambia yule mama, “Imani yako imekuponya”. Kwa upande wa mkuu wa sinagogi alimwambia, “usiogope, amini tu”. Imani inarudisha urafiki kati ya mwanadamu na Mungu. Imani inamfanya mwanadamu atambue kuwa bila Mungu hawezi kufanya kitu chochote kwa ukamilifu; anapojitenga na Mungu anakuwa na masuluhisho ya muda mfupi. Huo ndiyo mwarobaini anaotuletea Kristo katika jamii yetu leo hii. Pamoja na zawadi hii bado tunataadharishwa uwepo wa ukinzani kutoka kwa watu ambao wanatuzunguka. Wapo ambao kama mitume pamoja na kuwa karibu na Kristo wanashindwa kuona nguvu ya Kristo na kutaka jambo hilo lipite tu; wapo ambao kama wale ndugu kule nyumbani wanatucheka na kutudhiaki na pengine kutuona kama wendawazimu lakini Kristo anaendelea kutuambia: “usiogope, amini tu”.

Injili ya leo inatuonesha namna mbili zinazotufikisha katika kuionja nguvu ya Mungu ya uponyaji kwa njia ya imani. Kwanza ni kwa njia ya kupelekwa na na watu wengine. Hapa tunakumbushwa wajibu wetu wa kuombeana na kushirikishana utajiri wa kiroho kusudi kuufikia ukombozi tunaopewa kwa njia ya Kristo. Hii ni namna ambavyo tunaguswa na mahangaiko ya watu wengine na hivyo tunakuwa wajumbe wa kuufunua uso wa huruma ya Mungu kwao kwa sala zetu na maisha yetu ya ushuhuda. Pili ni pale tunapojongea sisi wenyewe kuindea huruma ya Mungu. Baada ya mahubiri, maelekezo na mifano mbalimbali kutoka kwa wapendwa wetu tunavutwa kwenda kwa Kristo. Namna hii ya pili inaonekana katika namna njema ya kugusa bila kujulikana lakini Yeye aonaye sirini atakuinua mwenyewe. Hapa inaonekana dhana ya unyenyekevu na subira katika kuujongea uponyaji wa Mungu. Namna zote hizo mbili zinachagizwa na paji la imani. Haya yote yanatudai unyenyekevu, subira na upole.

Wajibu wetu kama Wakristo unafafanuliwa zaidi na Mtume Paulo anapowaasa Wakristo wa Korinto juu ya umuhimu wa kutajirishana wao kwa wao ili mwishoni kusiwepo na aliyezidi au aliyepungua huku akimweka Kristo kama mfano: “aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala aliyekusanya vichache hakupungua”. Upendo huu wa kushibishana ni tunda la imani thabiti kwa Mungu. Mwanadamu atakapomweka mwenyezi Mungu kuwa sababu na chanzo cha yote aliyonayo upendo wake kwa Mungu utakua na hivyo ataiona sura ya Mungu katika nafsi ya ndugu yake. Kujifungua kiroho kwa wenzetu na kuwa tayari kuwaangazia wengine nguvu na uwezo wa Mungu na kwa njia hiyo tunaimarisha undugu kati yetu sisi kwa sisi na kujenga umoja madhubuti na Mungu muumba wetu. Mama yetu Bikira Maria, aliyechagizwa na imani thabiti kwa Mungu hata kuwa tayari kuitikia ‘ndiyo’ kwa wito wake na kutuletea mkombozi, yaani mwanae Yesu Kristo, atuombee.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.