2018-06-26 14:30:00

Ulinzi, usalama na maendeleo ya watoto yapewe kipaumbele cha kwanza


Bwana Valerio Neri, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la “Save the Children” anasema, tangu mwaka 1919, Shirika lake limekuwa mstari wa mbele kuokoa maisha ya watoto sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuwahakikishia leo na kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya elimu. Anasema, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inapaswa kushughulikiwa kwa kutoa kipaumbele kwa sera na mikakati ya kulinda watoto. Watoto wakimbizi na wahamiaji wamejikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu na viungo vyake!

Ni watoto ambao wako hatarini sana kuingizwa kwenye mifumo ya utumwa mamboleo, hali inayo dhalilisha utu na heshima yao kama binadamu! Kumbe, Mkutano wa Jumuiya ya Ulaya unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, hauna budi kutoa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa sera inayojikita katika: kuwapokea, kuwalinda na kuwashirikisha katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwakarimu!

Bwana Valerio Neri anasikitika kusema, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya imeshindwa kuwa na sauti na sera moja kuhusu wakimbizi na wahamiaji. Viongozi wa Ulaya wanaendelea kujiimarisha kwa kulinda mipaka ya nchi zao. Lakini, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Shirika la Kimataifa la “Save the Children” linawataka wakuu wa Jumuiya ya Ulaya kujizatiti zaidi katika kuibua mbinu mkakati na sera kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso na dhuluma! Wahakikishe kwamba, haki msingi za watoto hawa zinalindwa na kuheshimiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.