2018-06-26 09:19:00

Uhuru wa kidini ni msingi wa: haki, utu na heshima ya binadamu!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uhuru wa kidini ni kiini cha haki msingi za binadamu kinachompatia mwamini uwezo wa kufikiri na kutenda kadiri ya dhamiri yake nyofu na kwamba, haki hii ni chimbuko la utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhuru wa kidini unapaswa kuzingatiwa na kuendelezwa kisheria. Binadamu aliyeumbwa kwa akili na utashi kamili, anasukumwa na maumbile na kanuni maadili kuutafuta ukweli, kuuambata na kuushuhudia. Uhuru wa kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii na kati ya Mungu na binadamu.

Chuo kikuu cha Kipapa cha Santa Croce kilichoko mjini Roma kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji pamoja na Ubalozi wa Marekani mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 25 Juni 2018 kwa pamoja waliandaa Kongamano la Kimataifa kuhusu “Umuhimu wa kulinda uhuru wa kidini: kwa ushiriki na vitendo”. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika hotuba yake elekezi amekazia umuhimu wa uhuru wa kidini kama unavyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao la “Dignitatis humanae” yaani “Uhuru wa kidini”.

Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameendelea kutoa kipaumbele cha kwanza katika kukuza na kudumisha uhuru wa kidini dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani inayoendelea kusababisha mauaji ya kimbari, dhuluma na nyanyaso dhidi ta Wakristo huko Mashariki ya Kati na sehemu mbali mbali za dunia! Uhuru wa kidini unapaswa kulindwa na kudumishwa mintarafu Katiba na Sheria za nchi zinazotafsiriwa katika maisha ya kisiasa na kijamii.

Inasikitisha kuona kwamba, uhuru wa kidini ni jambo ambalo linataka kuwekwa pembezoni mwa maisha ya hadhara, ili kuonekana kana kwamba ni jambo la mtu binafsi. Dini zimetumiwa na baadhi ya viongozi kuchochea: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uhuru wa kidini usipozingatiwa na kuheshimiwa, matokeo yake ni vita na kinzani mbali mbali.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume “Ecclesia in Medio Oriente” yaani “Kanisa Mashariki ya Kati” anaonesha mateso, dhuluma na nyanyaso wanazokabiliana nazo Wakristo huko Mashariki ya Kati kutokana na utawala wa mabavu na kwa wakati huo, utawala wa Rais Saddam Hussein. Matokeo yake ni kuibuka na kuenea kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani; vita na ghasia kati ya watu; hali ambayo sasa imepelekea dhuluma, nyanyaso na mauaji ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hii ndiyo hali inayowakuta Wakristo huko Siria, Iraq, Misri, Uturuki na Lebanon. Hata katika nchi yao wenyewe, bado wanaendelea kujisikia kuwa ni “watu wa kuja” wageni na wapita njia”. Hawa kimsingi wanaendelea kujisikia kuwa ni raia daraja la pili, jambo ambalo si haki kabisa.

Kardinali Leonardo Sandri anakaza kusema: haki, amani, maridhiano na uhuru wa kidini hauna budi kukuzwa na kudumishwa na Jumuiya ya Kimataifa sanjari na  kulinda haki msingi za binadamu. Kilio na mahangaiko ya wananchi wa Siria ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Wakristo wanayo haki ya kubali nchini Iraq, ili kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi yao. Kardinali Leonardo Sandri amelishukuru Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji kwa mchango wake mkubwa katika kuyasaidia Makanisa yanayoendelea kuteseka, kudhulumiwa na kunyanyasika, ili yaweze kuendelea kujikita katika huduma kwa familia ya Mungu katika eneo hili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.