2018-06-26 06:36:00

Papa Francisko: Kilio cha familia ya Mungu Mashariki ya Kati ni kikali


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki,  ROACO kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, Baba Mtakatifu aliweka kando hotuba aliyokua ameandaa na kuanza kujikita zaidi katika kilio cha mateso ya watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, kiasi kwamba, kuna wasi wasi kuwa iko siku, Ukristo utafutika na kutoweka. Lakini, ikumbukwe bila Ukristo, hakuna utambulisho halalali wa uwepo wa Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwa uchungu mkubwa kwamba, leo hii, Mashariki ya Kati inateseka na kulia kwa uchungu, kiasi kwamba, kwa baadhi ya viongozi wakuu wa Mataifa, Mashariki ya Kati si tena kipaumbele cha sera na mikakati yao ya: kitamaduni, imani na maisha ya watu wa Mungu katika eneo hili. Wengi wao wanaiangalia Mashariki ya Kati kama mahali pa kujitwalia eneo la kutawala na kujichotea utajiri wake bila kumwaga jasho. Idadi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati inaendelea kudidimia kila kukicha na wengi wao, wamelazimika kuyakimbia makazi yao na wala hawana tena mpango wa kurejea huko, kwani mateso wanayokumbana nayo ni makubwa sana, kiaasi cha kuwakatisha tamaa!

Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu wenye imani thabiti, wanaipenda nchi yao, lakini mateso yamewazidi, kiasi cha kuwakatisha tamaa ya maisha. Mashariki ya Kati ni kiini cha Ukristo, mahali alipozaliwa, akateswa, akafa na kufufuka Kristo Yesu kutoka kwa wafu, limbuko lao waliolala katika imani. Ni eneo lenye utajiri na amana kubwa ya maisha ya kiroho, kitaalimungu, kitasaufi, likiturujia na hata kwa usanifu wa majengo. Ni eneo ambalo limesheheni Mababa wa imani, Waalimu wa Kanisa pamoja na umati mkubwa wa watakatifu wa Mungu. Huu ndio utajiri na amana inayofumbatwa huko Mashariki ya kati, kumbe, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, amana hii inatunzwa na kuendelezwa.

Baba Mtakatifu analishuruku sana ROACO kwa maisha na utume wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na huduma kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, katika kipindi cha miaka 50 ya uwepo na huduma. Mababa wa Kanisa kutoka Mashariki ya Kati wanafundisha na kukazia kwamba, taamuli makini ni chemchemi ya utakatifu wa maisha. Inasikitisha kuona kwamba, Mashariki ya Kati, limegeuka kuwa ni eneo la wakimbizi na wahamiaji; watu waliokata tamaa katika maisha. Huko Lebanon, sehemu kubwa ya wananchi wake ni wakimbizi na wahamiaji. Nchi ya Yordan inatoa hifadhi kwa idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Siria. Uturuki inatoa huduma kwa wakimbizi wengi wanaotoka Iraq.

Baba Mtakatifu anakumbuka kwa uchungu mkubwa hija yake ya mshikamano wa kiekumene aliyofanya kwenye Kisiwa cha Lesbos, Ugiriki, akiwa ameambatana na viongozi wakuu wa Makanisa nchini humo, akajionea mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji: Wakristo na Waislam, wote wakiwa wanateseka kutokana na madhara ya vita na misimamo mikali ya kiimani. Italia na nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya zimekuwa ni kimbilio la usalama na hifadhi ya wakimbizi na wahamiaji, changamoto kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga kwa njia ya mshikamano wa kimataifa unaoongozwa na kanuni auni.

Lengo msingi liwe ni kukomesha vita na ghasia, ili kutoa fursa kwa watoto kupata hata walau elimu ya msingi, huduma ya afya, ustawi na maendeleo endelevu! Lakini, ikiwa kama mvua ya mabomu itaendelea kuwanyeeshea watu wasiokuwa na hatia, ni vigumu sana kupata amani na utulivu huko Mashariki ya Kati! Baba Mtakatifu Francisko anasema, dhambi ya mauti huko Mashariki ya Kati ni vita! Hata waamini nao wanayo dhambi inayowatafuna pole pole!

Hii ni dhambi inayotenganisha imani na uhalisia wa maisha ya watu! Hawa ni baadhi ya wakleri, mashirika ya kitawa na hata waamini wanaotangaza ufukara, lakini katika uhalisia wa maisha yao ni watu wanaopenda anasa na utajiri, kiasi cha kusababisha kichefuchefu na hivyo kukosa mvuto na mashiko kama sehemu ya ushuhuda wa maisha ya imani inayomwilishwa katika matendo! Baba Mtakatifu anawataka wote wale ambao wameelemewa na kumezwa na maisha ya anasa na utajiri, kuanza kujiondoa huko, ili kwamba, kiasi cha mali na utajiri huu, uweze kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati!

Itakumbukwa kwamba, Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kunako mwaka 2017 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Tukio hili likapambwa kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Makanisa ya Mashariki. Kuanzia tarehe 19-22 Juni 2018 Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO limekuwa likiadhimisha mkutano wake wa 91 wa mwaka sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake rasmi. ROACO ni chombo cha matumaini ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo kwa sasa limegeuka kuwa uwanja wa vita. Jubilei hii ni kipindi cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu na wafadhili mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye shida mbali mbali katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.