2018-06-23 16:21:00

Papa Francisko: Makanisa Barani Afrika shikamaneni kwa dhati!


Muungano wa Makanisa Huru Barani Afrika, “the Organization of African Instituted Churches”, OAIC, ulianzishwa kunako mwaka 1978 kama Jukwaa la kuyaunganisha Makanisa mahalia ili kuweza kuwahudumia wanachama wake, kwa njia ya Neno la Mungu na ushuhuda unaomwilishwa katika maisha ya familia. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Muungano wa Makanisa Huru Barani Afrika na kuwashukuru kwa juhudi zao za kutaka kurejesha tena mahusiano na Kanisa Katoliki.

Muungano wa Makanisa haya umekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kudai uhuru Barani Afrika; kujenga na kudumisha haki na maani, ili kusimama kidete, kulinda, kutetea utu na heshima ya familia ya Mungu Barani Afrika. Inasikitisha kuona kwamba, matumaini ya maendeleo endelevu na haki yaliyokuwa yanatafuta kwa udi na uvumba, imebaki ndoto ya mchana kutokana na ukweli kwamba, Mataifa mengi Barani Afrika bado yanaendelea kuogelea katika vita, uchumi duni, migogoro na kinzani za kijamii na kisiasa; mambo ambayo hayatoi fursa kwa wananchi kucharuka katika maendeleo.

Mchakato wa uinjilishaji Barani Afrika, bado unakumbana na changamoto katika uinjilishaji, upatanisho na huduma ya maendeleo endelevu. Bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba, Barani Afrika amani na utulivu vinapatikana; watoto wanapata fursa ya kwenda shule na vijana wa kizazi kipya wanapata wao pia nafasi za kazi kwa kutambua vijana wanaunda sehemu kubwa ya idadi ya watu Barai Afrika.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Bara la Afrika leo hii ni kama mtu mmoja aliyeshuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa! Bara la Afrika lina kiu ya kusikiliza na kushuhudiwa Habari Njema ya Wokovu itakayowasaidia kupambana na umaskini, kwa kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wazee na wale wote wanaoteseka! Injili ya Kristo inayotangazwa na kushuhudiwa, haina budi kumwilishwa katika matumaini, amani, furaha, utulivu, upendo na umoja!

Matatizo na changamoto za Bara la Afrika zinaweza kupewa kisogo ikiwa kama raslimali watu, utajiri wa utamaduni na mali asili, vitatumika kikamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Dhamana na wajibu wa Kikristo ni kuhakikisha kwamba, raslimali na utajiri wote huu, unatumika kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; kwa kujikita katika mchakato wa amani katika maeneo ambamo mtutu wa bunduki bado unatawala na hivyo kutishia maisha. Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, kwa ajili ya huduma kwa maskini; kwa kuwawezesha hata waamini wenyewe kujikusanya na hatimaye, kujisadaka kwa ajili ya huduma na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahamisha viongozi wa Makanisa mbali mbali Barani Afrika, kuunganisha nguvu zao, ili kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha: uhuru, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wakristo washikamane kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, licha ya tofauti zao msingi za kitaalimungu na Kikanisa.

Familia ya Mungu Barani Afrika, kimsingi inafumbata tunu za maisha ya kiroho, kwani wao dini ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vyao. Wanatambua na kuthamini uwepo wa Mungu muumbaji sanjari na ulimwengu wa maisha kiroho. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; upendo kwa zawadi ya uhai na watoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni mambo msingi sana katika maisha ya watu wa familia ya Mungu Barani Afrika. Ujirani mwema na heshima kwa wazee ba watu wazima ni mambo msingi yanayopaswa kuigwa na jamii nyingine na kwamba, tunu hizi ni sehemu ya maisha na utambulisho wa Kikristo. Kwa njia ya tunu hizi msingi, waamini wanaweza kujenga na kudumisha mshikamano, mahusiano kati yao binafsi na jamii katika ujumla wake.

Viongozi wa Makanisa Barani Afrika, wawe mstari wa mbele kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa makabila, lugha, mila, tamaduni na dini mbali mbali, ili kuvunjilia mbali dhana ya uadui ambayo kwa miaka mingi imejengeka kati ya watu wa familia ya Mungu Barani Afrika. Kwa jinsi hii, kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene; ushirikiano na Makanisa yote pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam bila ya kuwasahau wale ambao bado wana amini katika dini za kijadi, kwa jili ya Afrika iliyo bora zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni.

Mwishoni, wa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Muungano wa Makanisa Huru Barani Afrika ambao wako mjini Roma kwa ajili ya kutembelea maeneo matakatifu, ili kukuza na kudumisha ari na moyo wa kiekumene, ili kujenga Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika haki, amani na udugu; mambo ambayo Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.