2018-06-23 16:53:00

Papa Francisko: Dumisheni udugu katika ujasiri, mabadiliko na nia!


Chama cha Wanafunzi Ndugu wa  Emouna, "Emouna Fraternité Alumni" kilianzishwa huko Paris, Ufaransa kunako mwezi Septemba 2016, kwa lengo na kutoa majiundo kamili kwa viongozi wa Ibada kuhusiana na masuala changamani na mtambuka mintarafu, serikali, haki, wajibu pamoja na uwezekano wa kushirikiana na dini mbali mbali ili kukuza na kudumisha haki, amani na utulivu. Chama hiki ni matunda ya programu iliyokuwa inaendeshwa na Taasisi ya “Emouna- L’Amphi de religion” kwa ushiriki mpana wa dini kuu zote zinazotekeleza dhamana na wajibu wake nchini Ufaransa.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Juni 2018 amekutana na wawakilishi wa Chama cha Wanafunzi Ndugu wa Emouna na kuwapongeza kwa jitihada za chama hiki ambacho pamoja na mambo mengine, kinapania kukuza na kudumisha udugu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali, kwa njia ya tafiti. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi hii kwa kuwawezesha watu katika tofauti zao msingi kuweza kuishi kwa amani, huku wakiheshimiana katika tofauti zao sanjari na tunu msingi za maisha yao ya kiroho.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba, mwelekeo huu unaonesha umuhimu wa dini kuhusishwa katika maisha ya hadhara katika jamii ambamo dini inaonekana kutengwa na kuwa kama kitu cha binafsi. Huu ni ushuhuda wa mshikamano wa kidugu unaoundwa na kujengeka kati yao, kiasi cha kuchochea mchakato wa majadiliano ya kidini baina ya waamini wa dini mbali mbali, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa amani duniani. Baba Mtakatifu amependa kuchukua fursa hii kuwatia shime kuendelea kujikita katika safari hii pamoja na kujitahidi kuunganisha mambo makuu matatu: Ujasiri; Mabadiliko na Nia Njema.

Udugu wa kweli unafumbatwa katika uwezo wa kushirikiana na kushikamana na wengine na kutambua kwamba, tofauti zao msingi ni tunu inayowatajirisha wote, ili kutambuana na kuheshimiana, ili kuboresha mahusiano na mafungamano yao. Watambue kwamba, dini si chanzo cha tatizo, bali ni sehemu ya suluhu ya matatizo mbali mbali yanayomwandama mwanadamu. Hapa kuna haja ya kuinua nyoyo juu, ili kuthubutu kujenga Mji wa Binadamu.

Kwa njia hii, anasema Baba Mtakatifu Francisko, wataweza kutembea bega kwa bega, huku wakiwa wamekita mizizi yao katika historia, tamaduni na hivyo kuchangia mchakato wa ujenzi wa udugu, unaobomolea mbali chuki na uhasama kati ya watu! Wajumbe hawa wanaendelea kuhamasishwa ili kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana; ili kujenga misingi ya amani sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utakatifu wa maisha ya binadamu dhidi ukatili wa kimwili, kijamii, kielimu au kisaokolojia. Wajumbe hawa waoneshe ujasiri wa kusali na kuombeana; waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwakirimia amani katika maisha; Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awawezeshe kutembea pamoja kama ndugu katika njia ya watu kukutana, kujadiliana; ili hatimaye, kuishi kwa utulivu unaofumbatwa katika moyo wa ushirikiano na urafiki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.