2018-06-22 17:12:00

Papa Francisko aonesha moyo wa shukrani nchini Uswiss!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha hija yake ya kichungaji, Alhamisi, tarehe 21 Juni 2018, akiwa njiani kuelekea mjini Roma, alipata nafasi ya kutuma salam na matashi mema kwa Rais Alain Berset wa Shirikisho la Uswiss. Katika salam zake, Baba Mtakatifu ameonesha moyo wa shukrani kubwa kwa familia ya Mungu nchini Uswiss kwa mapokezi ya “kata na shoka” pamoja na ukarimu wote waliomwonesha. Amewahakikishia sala na sadaka yake na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume!

Baba Mtakatifu alipokuwa anaingia kwenye anga la Italia, alimtumia salam na matashi mema, Rais Sergio Mattarella wa Italia, akionesha furaha ya kukutana na wawakilishi wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo huko Geneva, Uswiss kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ni Makanisa yanayoendelea kujizatiti katika majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kudumisha umoja na amani. Baba Mtakatifu anaitakia kila la kheri na baraka familia ya Mungu nchini Italia na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, amemtumia Baba Mtakatifu Francisko salam na matashi mema, kwa kumkaribisha tena, baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Uswiss, ambayo imeacha alama ya kudumu kama sehemu ya upyaisho wa mchakato wa imani katika majadiliano ya kiekumene, unaopania kuwahamasisha Wakristo kutafuta na kuambata mambo msingi yanayowaunganisha kama wafuasi wa Kristo Yesu. Anakaza kusema, dira na mwongozo wa majadiliano ya kiekumene yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko unaonesha dhamiri nyofu ya umoja na maridhiano kati ya watu kama nguzo msingi katika mchakato wa kupambana na changamoto mamboleo!

Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na ujumbe wake kurejea salama salimini mjini Roma, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kumshukuru Bikira Maria, Afya ya Warumi, kwa ulinzi na tunza yake ya kimama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.