2018-06-21 17:20:00

WCC: Ulimwengu uliomeguka unahitaji alama na ushuhuda wa nguvu!


Baada ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na Taasisi ya Kiekumene ya Bossey, Alhamisi tarehe 21 Juni 2018, kilichowajumuisha Baba Mtakatifu Francisko na ujumbe wake, viongozi wakuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na baadhi ya wanafunzi, ulifuatia mkutano wa kiekumene ambao ulifunguliwa kwa sala na hotuba kutoka kwa viongozi wakuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa Baraza la Makanisa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 70 ya uwepo na huduma katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kwamba, tukio hili linaweka kumbu kumbu ya kudumu.

Makanisa yanataka sasa kutembea, kusali na kuhudumia watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wakristo wanataka kukoleza majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja ili ulimwengu upate kusadiki. Hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha kwamba, kuna uwezekano wa kuvukwa utengano uliosababishwa na tamaduni pamoja na Mapokeo mbali mbali ya kiimani! Wakristo hawajafanikiwa kuwa na umoja kamili, ndiyo maana wanamwomba Roho Mtakatifu, awaongoze, awaunganishe na kuwasukuma kwenda mbele. Walimwengu waliogawanyika na kusambaratika, wanahitaji alama na ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

, kwa kulinda na kutunza maisha na mazingira nyumba ya wote; kwa kuepukana na vita, kinzani na mipasuko; ili kupunguza kama si kuondoa kabisa pengo kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi, unyonyaji, udhalilishaji wa utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi, ili kuwajengea watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya ni alama ya matumaini. Kwa muda wa miaka 70 Baraza la Makanisa Ulimwenguni limetembea, limesali na kuwahudumia watu wa Mungu bila kuchoka na kwamba, tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kumekuwepo na ushirikiano wa karibu zaidi kutoka katika Kanisa Katoliki.

Wakristo wanahimizwa na upendo wa Kristo Yesu kuwa ni wahudumu wa Upatanisho; wajenzi na vyombo vya: haki, amani na upatanisho; daima wakiongozwa na upendo wa Kristo, ili umoja wa Wakristo uweze kupatikana siku moja na kamwe wasiruhusu watu wachache kuvuruga mchakato huu. Majadiliano ya kiekumene yaendelee kujichimbia katika ukweli, uwazi na upendo; kwa kuthubutu kujisadaka, ili kweli umoja wa Kanisa uweze kuonekana.

Kanisa liendelee kuwa ni chombo cha upatanisho, haki na amani; huduma na utume unaowataka kutembea, kusali na kufanya kazi kwa pamoja. Wakristo ni mahujaji wa: Imani, matumaini na mapendo! Wanakiri Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi na kwamba, utume wao unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wakristo wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa kutafuta na kudumisha haki uchumi pamoja na kupambana na umaskini duniani, ili kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Malengo ya Maendeleo Endelevu sanjari na kusali kwa pamoja.

Kwa upande wake, Dr. Agnes Abuom, Mratibu wa Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni ambaye katika hotuba yake, amekazia Zaidi mshikamano, haki na amani mambo ambayo katika ulimwengu mamboleo yanamezwa sana na ubinafsi na uchoyo, uchu wa mali na madaraka. Sala ya Baba Yetu Uliye mbinguni, iwe ni dira na mwongozo wa hija ya Wakristo katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni muhtsari unaofumbata maisha ya Kikristo, matumaini kwa siku za usoni na wajibu wao katika kukuza na kudumisha: Injili ya uhai, haki na amani, sanjari na kuendelea kujikita katika upatanisho unaofumbatwa katika umoja na mshikamano.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, linataka kushirikiana na Baba Mtakatifu Francisko kwa karibu Zaidi kutembelea madonda ya watu waliojeruhiwa na wanaoteseka; kuadhimisha kwa pamoja zawadi ya maisha na kusonga mbele kupigania: haki, amani na upatanisho; ili kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baraza linaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini; kuibua na kupanga sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu; Haki mazingira, kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji na kwamba, kwa sasa Baraza linataka pia kujielekeza katika ushirikiano: ulinzi na huduma kwa vijana na watoto, kutokana na Kanisa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa vijana na kwa mwaka huu, kuadhimisha Sinodi ya Vijana.

Dr. Agnes Abuom anasema, kumekuwepo na mafanikio makubwa miongoni mwa Makanisa katika kutafuta haki, amani na upatanisho Kusini mwa Sudan, Colombia, Korea na kwamba, bado Makanisa yanapaswa kujifunga kibwebwe ili amani iweze kupatikana huko Burundi, DRC na Sudan ya Kusini. Wakristo wakiendelea kutembea, kusali na kushirikiana wanaweza kutenda makubwa zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.