2018-06-20 09:30:00

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji na changamoto zake kimataifa!


Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kuweza kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linaloendelea kuwagawa viongozi wa Umoja wa Ulaya. Hawa ni watu wanaotafuta; hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kuliko kule walikokuwa wanaishi. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano, ili kusikiliza na kujibu kwa vitendo kilio cha wakimbizi na wahamiaji; changamoto ambayo kwa sasa inapigwa danadana!

Ushirikiano huu ujengeke kuanzia kule wanakotoka wakimbizi na wahamiaji, katika nchi zile wanamopitia hadi mwisho wa safari yao. Pale hali na mazingira yanaporuhusu, basi, wakimbizi na wahamiaji waweze kurejea tena kwa uhuru na usalama kwenye nchi zao za asilia. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuongozwa na dhamiri nyofu, ili kuweza kutoa majibu muafaka ya changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Hawa kwa hakika ni watu wanaopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuthaminiwa utu na heshima yao kama binadamu.

Ikumbukwe kwamba, baadhi yao ni waathirika wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo! Wengine ni wale wanaotoka katika maeneo ya vita, ghasia, nyanyaso na dhuluma bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika ujumbe alioiandikia familia ya Mungu nchini Italia anasema, ameguswa na maneno ya Baba Mtakatifu Francisko anayewaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama sehemu ya mchakato wa utakatifu wa maisha.

Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Leo hii kuna njaa na kiu ya haki na amani; changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini kwa kushirikiana na wadau mbali mbali! Haki na amani haitaweza kudondoka kama manna jangwani na kama ilivyo kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kumbe, hapa kuna haja ya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchakarika kwa kujifunga kibwebwe ili kupambana na hali pamoja na mazingira yanayosababisha kutoweka kwa misingi ya haki na amani sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema, kwa hakika anatambua fika: matatizo, changamoto na fursa zilizopo kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Lakini, inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa ambao tayari wana majibu mepesi mepesi mifukoni mwao na kusahau kwamba, hii ni changamoto changamani inayopaswa kushughulikiwa kimataifa kwa kuwajibika barabara, kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kila mtu anayo haki ya kubaki nchini mwake bila kulazimika kuikimbia! Pale inapotokea kwamba, kuna watu wanalazimika kuzikimbia nchi zao, Kanisa linawajibika kuwasaidia kwa hali na mali, kwa kuzingatia misingi ya haki, umoja na mshikamano wa familia ya Mungu katika ujumla wake.

Ni matumaini ya Kardinali Bassetti kwamba, wanasiasa, vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, vitasaidia kutangaza ukweli, badala ya kuwajengea wananchi hofu na mashaka yasiyokuwa na mvuto wala mashiko. Jamii inapaswa kuwekeza katika elimu makini, ili kuvunjilia mbali: mawazo mgando, maamuzi mbele na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kanisa linakiri na kufundisha kuhusu utakatifu wa maisha ya binadamu unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, wanapaswa kuokolewa ili wasizame na kupotea kwenye kilindi cha Bahari ya Mediterrania ambayo imegeuka kuwa ni kaburi lisilokuwa na alama kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Injili ya uhai haina budi kulindwa na kudumishwa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Maisha haya yanapaswa pia kulindwa kwenye ofisi, jangwani na kwenye bahari wanakosafiri wahamiaji hawa kwa matumaini ya kupata hifadhi na usalama.

Utu na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji, kama ilivyo pia kwa wafanyakazi, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote, kila wakati, popote na daima. Familia ya Mungu nchini Italia katika changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, ilijipambanua kuwa ni nchi ya watu wenye ukarimu, upendo na mshikamano, inapaswa pia kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, katika kuwahudumia na kuwapatia hifadhi watu hawa. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwamba,  Jumuiya ya Ulaya itaweza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Italia katika kuokoa maisha ya watu hawa, kwa kuwajibika barabara. Kanisa litaendelea kuwa bega kwa bega katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, huku likitumaini kwamba, iko siku, amani na utulivu vitaweza kurejea tena katika Ukanda wa Mediterrania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.