2018-06-19 14:37:00

Jubilei ya Miaka 70 Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Ushuhuda na huduma


Hija ya Kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Geneva, huko nchini Uswiss hapo tarehe 21 Juni 2018, inaongozwa na kauli mbiu “Kutembea, Kusali na Kushirikiana” muhtasari wa dhamana na malengo makuu ya majadiliano ya kiekumene kwa wakati huu! Majadiliano ya kiekumene ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha amani, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia! Hizi ni juhudi zinazolenga kutoa ushuhuda wa Makanisa katika kusimamia: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kujikita katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Miaka 70 iliyopita yaani kunako mwaka 1948, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. lilianzishwa likiwa na Makanisa wanachama 147 na tangu wakati huo, zaidi ya Makanisa 200 yamejiunga na kuwa ni sehemu ya Baraza hili yakiwa na waamini zaidi ya milioni 560. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki ni mjumbe mtazamaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kumbe, Jubilei ya Miaka 70 ya uwepo na utume wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya Makanisa duniani. Hili ni tukio ambalo litaendelea kuboresha mahusiano kati ya Makanisa katika ngazi mbali mbali, ili siku moja, Wakristo wote wawe chini ya Mchungaji mmoja, Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika maadhimisho Ibada ya Jubilei ya miaka 70 ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Jumapili tarehe 17 Juni 2018, huko Geneva anasema, majadiliano ya kiekumene ni mchakato endelevu unaowataka Wakristo kujikita katika toba na wongofu wa ndani; ili kuachana na ukale, tayari kuanza kuangalia mambo kwa mwelekeo mpya zaidi! Ni mchakato unaohitaji uvumilivu na moyo mkuu pasi na kukata tamaa kutokana na vizingiti mbali mbali vinavyoendelea kuibuka duniani.

Umoja wa Wakristo duniani, kinapaswa kuwa ni chombo makini cha kujibu changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwaliko wa kujibu kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita, njaa, umaskini na maradhi. Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia imani katika matendo kama ilivyokuwa wakati wa Mwaka 1920. Hii ni fursa kwa Wakristo kujikita katika mchakato wa haki, amani, upatanisho na mshikamano; mambo makuu yanayofumbatwa katika Habari Njema ya Wokovu

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kunako mwaka 1948, kumekuwepo na mabadiliko na changamoto nyingi ndani ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, lakini Makanisa hayana budi kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Lengo ni kuvuka vikwazo na vizingiti vinavyojitokeza; kutubu na kuongoka, ili kuachana na maamuzi mbele, mila na tamaduni ambazo zilipelekea Kanisa kusambaratika, ili hatimaye, Wakristo waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda amini wa Habari Njema ya Wokovu. Majadiliano ya kiekumene ni jukwaa linaloyawezesha Makanisa kukutanisha tofauti zao za: kitasaufi, kitaalimungu na kiliturujia ili kuwa na mwelekeo wa kikatoliki wa Kanisa; kwa kujikita katika mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo, kuliko yale yanayowagawa na kuwasabambaratisha, ili kujenga umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, umefika wakati kwa Wakristo kutoka katika nchi, mila na tamaduni mbali mbali kuungana ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wajiweke chini ya ulinzi, tunza na uongozi wa Roho Mtakatifu na kumwachia nafasi, ili atende kadiri anavyoona inafaa. Ikumbukwe kwamba, Kanisa haliishi kwa ajili ya ustawi na mafao yake binadamu, bali linaitwa na kutumwa kuganga majeraha ya walimwengu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. limekuwa mstari wa mbele kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baraza limeendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na Makanisa mbali mbali duniani, lakini zaidi kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. limekuwa ni jukwaa la kushirikishana: utajiri, amana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu. Limeendelea kudumisha mapokeo ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo  sanjari na kudumisha uekumene wa maisha ya kiroho; uekumene wa damu, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.