2018-06-18 09:00:00

Papa: Katika magumu na giza la maisha, ndio wakati wa kukamatia imani!


Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 17 Juni 2018, amefafanua kuhusu ukuaji wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kristo Yesu, kwa njia ya mahubiri na matendo yake, alitangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu na kuupanda duniani. Kama mbegu iliyopandwa ardhini, Ufalme wa Mungu unakua na kupanuka kwa nguvu zake wenyewe, tofauti kabisa na matarajio binadamu. Ufalme unakua na kupanuka ndani ya historia na wala hautegemei sana kazi ya binadamu, bali ni kielelezo cha nguvu na wema wa Mungu sanjari na nguvu ya Roho Mtakatifu anayeyaongoza maisha ya Kikristo miongoni mwa watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wakati mwingine, historia na makando kando yake; wadau na wahusika wake wakuu, wanaweza kuonekana kana kwamba, wanakwenda kinyume cha mpango wa Mungu, anayetaka watoto wake wote wapate: haki, wajenge udugu na kuishi kwa amani. Waamini wanahimizwa kuishi vipindi vyote hivi kama sehemu ya majaribio ya matumaini na ujio wa siku ya mavuno. Kimsingi, kama ilivyokuwa jana na hata leo hii, Ufalme wa Mungu unaendelea kukua duniani kama fumbo linalowashangaza wengi pamoja na kuendelea kufunua nguvu yake iliyojificha katika mbegu ndogo; lakini inaonesha ile nguvu yake ya ushindi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika madonda ya maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake, yanayoonekana wakati mwingine kutaka kuzamisha meli ya matumaini, kuna haja ya kujizatiti kuendelea kuwa na imani, katika utekelezaji na nguvu ya Mwenyezi Mungu. Wakati wa patashika nguo kuchanika katika maisha ya imani, pale mwamini anapokumbana na giza nene katika maisha yake pamoja na kusongwa mno na matatizo ya duniani, hapo ndipo anapopaswa kuonesha uaminifu wake kwa Mwenyezi Mungu, kwani uwepo wake, daima unaokoa, kwani Mungu ni mwokozi.

Katika mfano wa pili, Yesu anaulinganisha Ufalme wa Mungu kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, si rahisi sana kuona mantiki ya utendaji wa Mungu na kuipokea katika uhalisia wa maisha. Lakini, waamini wanahamasishwa kujikita zaidi katika imani inayovuka mipango yao, mahesabu na matarajio yao.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu, daima ni Mungu anayeshangaza, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufungua nyoyo zao na kupokea kwa ukarimu mpango wa Mungu katika maisha yao, iwe ni katika ngazi ya mtu binafsi au ngazi ya kijumuiya. Mwenyezi Mungu anatumia matukio ya kila siku kuwashirikisha waja wake: upendo, ukarimu na huruma kwa watu wote pasi na ubaguzi!

Ukweli wa utume wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu haufumbatwi katika ufanisi na matokeo makubwa, bali ni kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, kwa ujasiri, imani na unyenyekevu, huku likijiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Ni mchakato wa kusonga mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Wakristo watambue kwamba, wao ni vyombo vidogo na dhaifu mikononi mwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa njia ya neema, wanaweza kutekeleza mambo makubwa, kiasi cha kusongesha mbele mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Bikira Maria awasaidie waamini kuwa wanyenyekevun na makini ili kuweza kushiriki kwa njia ya imani yao na kazi zao katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu katika nyoyo za watu na historia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.