2018-06-18 15:38:00

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa mashuhuda wa urithi wa imani


Waamini wanapaswa kuwa macho na makini kuhusu kishawishi cha kupenda mno madaraka kiasi hata cha kujisahau na kuanza kukanyaga haki msingi za wanyonge katika jamii. Mawasiliano tenge yanayolenga kuchafua wengine ni hatari sana katika jamii kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa, kiasi hata cha kufikia kiwango cha mauaji ya kimbari, kama ilivyotokea kwa Waisraeli. Kashfa ambayo hata leo hii bado inaendelea kumeng’enyua maisha ya watu! Kuna baadhi ya watu wanaotaka kujijenga katika medani mbali mbali za maisha, wanatumia vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya ustawi na mafao ya binafsi.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Juni 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu ameupongeza ushupavu ulioneshwa na Nabothi Myezreeli aliyekataa kumpatia Mfalme Ahabu wa Samaria shamba la urithi wa baba zake. Kwa masikitiko makubwa, Mfalme Ahabu, akawa na moyo mzito, akakasirika na kujilaza kitandani pake na kukataa kula chakula. Lakini Yezebeli mkewe, akataka kumshikisha adabu Nabothi, kwa kuandika nyaraka za tuhuma za kughushi kwamba, amemtukana Mungu na mfalme na matokeo yake akapigwa mawe hadi kufa! Mfalme Ahabu akainuka na kutamalaki shamba la mizabibu la Nabothi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Nabothi anakuwa ni shuhuda wa uaminifu kwa urithi kutoka kwa wazazi wake, ni urithi ambao aliweza kuhifadhi katika sakafu ya moyo wake!

Kuna uwiano mkubwa wa simulizi hili na mateso pamoja na kifo cha Kristo Yesu, Stefano Shahidi, wafiadini na mashahidi wengi ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya: uaminifu, imani na matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu. Hali kama hii, inatendeka hata katika ulimwengu mamboleo, kwanza kwa kusema, uwongo, baadaye mtu anahukumiwa na adhabu inatolewa! Lakini, yote haya ni mambo ambayo yanafumbatwa katika uwongo. Kuna baadhi ya viongozi wanaowanyima raia wao uhuru wa kujieleza, hali inayodhohofisha demokrasia shirikishi na matokeo yake, wananchi wanafungwa midomo na utawala wa mabavu, unazidi kushamiri na kutanua!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, leo hii hata vyombo vya mawasiliano ya jamii vimekuwa vikichakachua habari kwa kutangaza habari za kughushi na wala kwao habari za ukweli na maendeleo endelevu ya binadamu, hazina mashiko! Ni vyombo vinavyoshabikia habari za udaku na kashfa za kijamii, ili kufurahia watu kuanguka na kupotea katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii. Hivi ndivyo ilivyotokea hata kupelekea mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi. Hata leo hii, bado kuna watu wanakosewa haki zao kama Nabothi kwa kubambikizwa kesi za uwongo. Watu hawana nafasi ya kusikiliza ukweli, lakini wako tayari kutoa hukumu, ya kifo, kwa watu kutwangwa mawe!

Vyombo vya mawasiliano ya jamii havina budi kuwa makini katika kutoa habari badala ya kusababisha kinzani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Ulimi ni kiungo hatari sana, kinapaswa kudhibitiwa, ili kuboresha mawasiliano kama anavyokaza kusema, Mtume Yakobo katika nyaraka zake. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake, kwa kuwataka waamini kujitaabisha tena kusoma historia ya Nabothi inayopatikana kutoka katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme, Sura ya 21, ili kuona jinsi ambavyo watu, nchi na mataifa mengi, yamesambaratika kutokana na uwongo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.