2018-06-16 16:13:00

Papa Francisko: watawa jengeni umoja na udugu; umbea hauna tija!


Watawa wa Shirika la Teatine wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka mia nne, tangu Mtumishi wa Mungu Orsola Benincasa alipofariki dunia. Ni shirika ambalo linaendelea kujenga ufalme wa Mungu huko: Amerika, Afrika na Ulaya. Watawa hawa wanashirikiana kwa karibu sana na Mapadre wa Teatini, waliokabidhiwa na Mama muasisi wa Shirika kuwatunza kabla ya kifo chake.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 16 Juni 2018 alipokutana na kuzungumza na wa Watawa wa Shirika la Teatine wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili pamoja na Mapadre wa Teatini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mtumishi wa Mungu Orsola Benincasa alikuwa ni mwanamke wa taamuli, kiasi kwamba, alijisikia kuvutwa na Mwenyezi Mungu; akajitahidi kumwiga Kristo Yesu aliyeteswa. Ni mtawa aliyekuwa na Ibada ya Kuabudu Sakramenti kuu na kwake, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ikawa ni kiini cha maisha na chakula chake cha kiroho. Alivutwa sana na mwanga wa Fumbo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kiasi kwamba, karama ya Shirika lake ikaichimbia kwa Kristo Yesu na Bikira Maria; kama ushuhuda hai wa upendo usiokuwa na makuu.

Kutokana na mwelekeo huu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, akapata nguvu ya kujisadaka kwa ajili ya kujibu kilio cha maskini, hususan vijana, na akayafanya yote haya kwa ajili ya sifa, utukufu wa Mungu na wokovu wa mwanadamu! Kristo Yesu akawa nguvu ya maisha na sala za watawa wake kila siku ya maisha yao; ili kupenda walimwengu kwa moyo wa Kristo mwenyewe; kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili elimu na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya sanjari na kushiriki katika mchakato wa maendeleo na ukuaji wao kiimani!

Ni karama ambayo imewawezesha kuwa karibu na wagonjwa kwa njia ya huduma makini na hapo, wakawa na ujasiri wa kumtambua Kristo Yesu aliyesulubiwa. Leo hii, watawa hawa wanaitwa kutoka huko walikojichimbia, ili kuelekea na kuambata mambo msingi ya maisha kwa moyo ulio huru kabisa. Baba Mtakatifu anawataka wawatawa hawa kwa kuiga mfano wa mwanzilishi wao wa Shirika kujitahidi kuwa waalimu wa uwepo wa Mungu kati ya watu wake, kwani leo hii walimwengu wanahitaji mashuhuda watakaokuwa kweli ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Hii ni huduma muhimu sana, kama kilivyo chakula kwa mwili, kwani leo  hii watu wengi wamepoteza uzuri na maana ya maisha; wamekuwa na shingo ngumu.

Lakini bado kuna watu wenye njaa na kiu ya maji ya uzima, wanataka kukutana na kuonana na Kristo Yesu katika maisha yao. Ikiwa kama watakuwa wazi na wasikivu, Roho Mtakatifu ataweza kuwaongoza ili kujibu kilio hiki kwa ubunifu wa hali juu kabisa; kwa kukesha ili kuamsha matumaini miongoni mwa watu wa Mungu. Ulimwengu mamboleo anasema Baba Mtakatifu unahitaji mashuhuda wa maisha ya kidugu katika Jumuiya, kwa kuongozwa na tasaufi ya umoja kati yao, ili kwa pamoja waweze kujikita katika hija takatifu kwa kuondokana na misigano, umbea, kinzani, chuki na hasira, mambo ambayo kamwe hayana tija katika maisha ya kitawa. Watawa wajenge ari na moyo wa ukarimu, kusaidiana na kujaliana; kwa kushirikishana na kugawana karama, mapaji na zawadi wanazokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao; daima wakijitahidi kuheshimiana na kuthamiana kama ndugu.

Watawa wapendane na daima wajitahidi kutafuta mafao ya jirani zao na kwa njia hii, wataweza kumwilisha Amri kuu ya Upendo katika uhalisia wa maisha na utume wao: huko shuleni, kwenye parokia, hospitalini na mahali popote pale wanapotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa njia hii, watawa wataweza kujenga umoja, upendo na mshikamano ndani na nje ya Shirika lao. Baba Mtakatifu anawataka waendelee kusonga mbele kwa ajili ya huduma kwa maskini; kwa kuonesha uwepo wao pale penye shida kama watawa waliojiweka wakfu kwa ajili ya Mungu na jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.