2018-06-15 08:09:00

Ufalme wa Mungu: Unakua pole pole na kuzaa matunda kwa wakati wake!


Ndugu mpendwa katika jumapili ya XI ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tunatafakarishwa na mifano miwili – mbegu inayoota yenyewe na mbegu ya haradali. Mifano hii yaonesha mwelekeo wa ukuaji wa ufalme wa Mungu au namna ufalme wa Mungu unavyokua. Yesu anaposema ufalme utakua – anamaanisha kuwa ufalme hata kama unahitaji ushirikiano wetu, awali ya yote huhitajika neema na zawadi toka kwa Mungu. Siyo matunda ya nguvu za kibinadamu.

Katika somo la kwanza, Nabii Ezekieli anaongea kuhusu ukombozi wa taifa la Israeli. Anaongea wakati taifa likiwa utumwani. Anawaimarisha. Anasema, hata mti mkavu utastawi. Anatoa matumaini kwa taifa la Israeli. Ukuaji wa ufalme ni kazi yake Mungu na mwanadamu hawezi kuzuia. Yule anayetambua mapenzi yake Mungu anaitwa kushiriki kikamilifu katika ukuaji huo. Maisha ya hadharani ya Yesu na kwa namna ya pekee katika injili ya Matayo yanatanguliwa na hotuba kuu tano na kila moja ikitanguliwa na shughuli mbalimbali za Bwana ikiwepo miujiza. Lengo kuu likiwa ni kuweka wazi vipengele vya ufalme wa Mungu, ambalo ndilo lilikuwa jukumu la kwanza la Bwana. Kwa kifupi, ufalme huu wa Mungu ni ufalme wa upendo na amani na usiotawaliwa na aina yo yote ile ya dhambi.

Katika Agano Jipya, ufalme wa Mungu unaonekana katika ukamilifu wake siku za mwisho. Hii inajidhihirisha pale Yesu anaposema katika Marko 1:15 – akisema, wakati umefika, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini injili. Hapa Bwana Yesu alimaanisha habari ya ule ukamilifu ulio katika ufunuo wa Mungu Baba. Wakristo wa mwanzo, baada ya ufufuko wa Yesu, walitambua kwamba ufalme umekaribia katika Kristo mwenyewe na katika ujumbe wake. Hata hivyo walikwazwa na kutokuamini kwa watu wote na hivyo ikabidi wawekeze matumaini yao katika ujio wa pili wa Kristo. Lakini katika kipindi kati ya ufunuo wa kwanza na ule wa pili, mambo mengi yalitakiwa kufanyika. Yesu alisia mbegu na wafanyakazi walihitajika. Ule ujumbe wa ufalme wa Mungu uliotangazwa na Kristo, ulitakiwa uenezwe kwa ulimwengu mzima.

Mwinjili Mathayo anaona hili likifanywa na kanisa na amepanga hizo hotuba tano kwa namna ambayo unaonekana uhusiano wa wazi kati ya ufalme wa Mungu na uenezwaji wake ukifanywa na kanisa. Kwa mfano katika hotuba ya kwanza –hotuba ya mlimani – tunapata mwongozo mzima wa namna ya kuupata ufalme wa Mungu, namna ya kuupata ufalme katika kanisa. Kanisa lina wajibu wa kuutangaza ufalme huo.

Hapa inaingia nafasi yetu sisi wana kanisa katika ujenzi wa ufalme huo. Katika nafasi na tafakari ya dominika hii tunakumbushwa tena kazi ya uumbaji ambayo Mungu amemshirikisha mwanadamu. Nafasi yetu katika ujenzi wa huo ufalme iko wazi ila tunakumbushwa kubaki katika ushirika na Roho Mtakatifu. Yesu alipoita wafuasi aliwaalika kushiriki naye na hata baada ya safari yake ya mwisho hapa duniani anawakabidhi waeneze habari ya ufalme huo ulimwenguni kote. Siku ya kupaa kwake, ndiyo siku alipowakabidhi rasmi utume huo. Tukumbuke kuwa Mungu hufanya kazi pamoja nasi katika kuufanya ulimwengu huu mbingu ndogo.

Tutafakarishwe na mfano wa mtoto mdogo wa darasa la tatu anayeingia katika ugomvi na watoto wenzake lakini wa darasa la sita. Akibaki katika msimamo wake, yule mdogo anachora mstari kwenye udongo na kusema kuwa kama yupo anayethubutu basi ana auruke ule mstari aingie upande wake. Kwa sababu ya kiburi cha ukubwa na kuona kudharauliwa, wale wakubwa wakavuka ili kuona huyu bwana mdogo atawafanya nini. Baada ya kuvuka, yule mdogo akawacheka sana na kuwaambia sasa mko upande wangu. Wakawa marafiki. Ugomvi ukaisha. Mungu anatuita tuingie upande wake.

Kiburi chetu na hali yetu ya kibinadamu itapata maana ikiongozwa na Roho yake Mungu. Kwa namna hiyo, mbegu ya Mungu iliyosiwa ndani mwetu itapata kukua na kuzaa matunda. Mifano hii ya mbegu katika jumapili hii ni juu ya ukuaji wa ufalme wa Mungu ambao ndiyo kiini cha fundisho la Kristo. Tukiyatimiza mapenzi yake Mungu, tayari tunashiriki katika ukuaji wa  ufalme wa Mungu.

Sifa za ufalme wa Mungu ni hizi: uongofu na toba, uanachama hai, yaani kuwa pamoja na Kristo na kujifunza daima toka kwake,  kuwa wafuasi na watumishi waaminifu, utumishi wa kimapendo ukiongozwa na pendo lake Mungu na kuishi sheria ya msingi inayojengwa na maisha mapya katika Roho. Ni ile sheria ya kuwa watoto wake Mungu. Ni tabia au hali ya kuwa na maisha ya heri – Mt. 5:1-12.  Ili kushiriki katika ujenzi wa ufalme huu zipo njia nyingi na baadhi yake ni hizi: heshima kati yetu, mshikamano na maskini, uaminifu kwa Mungu na kati yetu na maisha ya ushuhuda.

Je, sifa hizi kama upendo, huruma, msamaha na upatanisho zipo kati yetu? Hizi ndizo mbegu hai. Hizi ndizo hali zinazotakiwa kuonekana na kukaa kati yetu. Hizi ndizo mbegu hai ambazo Yesu atualika leo kuwa nazo ili ufalme uweze kukua. Kama mfuasi wa leo wa Kristo unasaidiaje wengine kukua kiimani? Kama mimi na wewe tunashiriki kiaminifu katika kueneza Imani hai ya kikristo basi tuwe na uhakika kuwa tunashiriki katika ujenzi wa ufalme huo. Hatuko mbali na ufalme wa Mungu. Katika somo la pili, mtume Paulo anaonesha wazi kilichowapata Waisraeli huko utumwani. Anawaalika wafuasi/wana kanisa kutoka utumwani, katika hali ya dhambi na hali ya kifo na kuingia maisha mapya, maisha ya uzima. Tukiwa katika hali hii mpya inakuwa rahisi kushiriki kiaminifu katika ujenzi wa huo ufalme. Ile mbegu ya Imani iliyosiwa ndani yetu itakua na kuenea ulimwenguni kote.

Tumsifu Yesu Kristo.

PadreReginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.