2018-06-15 11:36:00

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Salam za Id Al Fitri kwa Waislam


Ramadhani au ramadan, ramazani (kwa Kiarabu رمضان) ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya dini ya Kiislamu na mwezi wa kufunga katika Uislamu kuadhimisha ufunuo wa kwanza wa Qurani kwa Muhammad. Mwezi huu huwa na siku 29 au 30 kutegemeana na kuandama kwa mwezi. Kufunga ni moja ya Nguzo Tano za Uislamu. Mwislamu mzima, mwenye afya nzuri, anatakiwa kushiriki katika swaumu ambayo ni ibada ya kufunga chakula na kinywaji mchana kutwa, pamoja na kujizuia kufanya mapenzi toka alfajiri hadi magharibi. Matendo hayo ya toba yanaendana na kuswali sana na kusoma Quran kwa wingi.

Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika salam zake za Id Al Fitri kwa waamini wa dini ya Kiislam, baada ya kuhitimisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, anasema, bila shaka mwezi huu umekuwa wenye manufaa na kipindi cha rehema kwa waamini wa dini ya Kiislam. Sasa ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha waamini wa dini mbali mbali kuungana kusherehekea neema ukarimu wa Mungu kwa waja wake, sanjari na kuganga na kuponya madonda ya: kinzani, uchoyo na mipasuko ya aina mbali mbali.

Hiki kimekuwa ni kipindi cha: kufunga na kuswali; toba na kutoa sadaka kama njia ya kumwilisha huruma na ukarimu wa Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linashukuru na kupongeza umoja na mshikamano unaoendelea kuoneshwa na wadau mbali mbali wa dini ya Kiislam, licha ya changamoto kubwa zilizoko mbele yao! Jambo la msingi ni kuendelea kukuza na kudumisha umoja, mshikamano pamoja na kuaminiana, ili kutangaza na kushuhudia misingi ya haki na amani katika Jumuiya za waamini. Majadiliano hayana budi kumwilishwa katika mchakato wa ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dr. Tveit anasema, tarehe 25 Juni 2018 Baraza la Makanisa Ulimwenguni litaadhimisha Kongamano la Kwanza la Kimataifa linaloongozwa na kauli mbiu “Dini, Kanuni ya Imani au Tunu msingi, Kuunganisha nguvu ili kudumisha usawa wa haki za uraia”. Kongamano hili limeandaliwa kwa ufadhili wa Mfalme El Hassan Bin Talal wa Yordan. Kongamano hili ni mwendelezo wa mdahalo uliofanyika kati ya Wakristo na Waislam kuhusu umuhimu wa kujizatiti katika mchakato wa haki sawa za uraia, ulioandaliwa na Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Uswiss, mwaka 2017.

Kongamano hili linalenga kuunganisha nguvu za kidini, kanuni za imani na tunu msingi za maisha ya kiroho ili kugaribisha mchakato wa haki sawa za uraia, kwa kuzingatia kanuni ya utofauti, usawa na ushirikishwaji. Itakumbukwa kwamba, mahusiano ya dhati kabisa kati ya Waislam na Wakristo ni muhimu katika kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani duniani. Huu ni wajibu mzito sana kwa waamini wa diini hizi mbili. Haki sawa za uraia ni chombo madhubuti katika mapambano dhidi ya woga usiokuwa na mashiko, ubaguzi na hali ya kutovumiliana; mambo yanayoendelea sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kuchafua na kuvuruga misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Ni wakati muafaka wa kuvunjilia mbali woga na wasi wasi unaojitokeza katika masuala ya kisiasa kwa misingi ya ubaguzi na utengano. Vitabu Vitakatifu vya dini hizi mbili vinahimiza moyo wa upendo na ukarimu unaofumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kiini cha Siku kuu ya Id Al Fitri ni kuwakumbusha waamini wa dini ya Kiislam tunu msingi za maisha ya kiroho zinazofumbatwa katika: nidhamu, mshikamano, huruma na upendo. Kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, waamini wa dini ya Kiislam walifunga na kutamani tunu za haki na amani. Mwishoni, Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika salam zake za Id Al Fitri kwa waamini wa dini ya Kiislam anawatakia wote mshikamano, huruma na upendo, wale wote wanaowazunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.