2018-06-14 15:17:00

Askofu Msonganzila: Changamoto za kichungaji zikabiliwe Kisinodi!


Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani "Kuhusu Shughuli za Kimisionari", Kanisa mwezi Oktoba 2019 linataka kutangaza Injili ya Kristo; Kuadhimisha vyema Sakramenti za Kanisa na Kutolea Ushuhuda makini wa imani inayomwilishwa katika matendo. Ni muda muafaka wa kujizatiti katika kuyategemeza Makanisa mahaliakwa kukazia majiundo awali na endelevu ya wamissionari; umoja na mshikamano kwa Makanisa Mahalia kwa kuunganisha nguvu katika masuala ya: familia, uzazi na malezi bora; Injili ya uhai; elimu na shule; pamoja na kuendelea kujikita katika kuwalinda watoto wadogo, kwa kusaidia majiundo makini ya wazazi na walezi; mapadre, watawa na makatekista!

Ili kuweza kupambana na changamoto zote hizi, kuna haja ya kujikita katika “Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, ili kuwawezesha watu wa Mungu kutembea kwa pamoja. Familia ya Mungu nchini Tanzania inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara inataka kukabiliana na changamoto za uinjilishaji kwa moyo wa umoja na mshikamano kama familia ya Mungu inayowajibika

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, katika mahojiano maalum na Vatican News anakaza kusema! Bado kuna changamoto nyingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa awali unaokwenda sanjari na uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, changamoto ambayo Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendelea kuivalia njuga “hadi kieleweke”. Hizi ni changamoto za kiimani zinazopambana na: mila, desturi na tamaduni potofu; mazingira magumu na hatarishi; hali ngumu ya kiuchumi inayokwamisha pia masuala mengi ya kiuchumi! Bado kuna maadui wa kitaifa yaani: ujinga, umaskini na maradhi.

Askofu Msonganzila anapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushuhuda wa uelewa mpana unaoendelea kutolewa na mihimili mbali mbali ya Uinjilishaji nchini Tanzania yaani: wakleri, watawa, makatekista pamoja na familia, shule ya kwanza ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni. Changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikiwa kwa umoja na mshikamano wa Kikanisa unaofumbatwa katika “dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Hii ni chachu muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya.

Kumbe, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sinodi katika ngazi mbali mbali yaani kuanzia ngazi za Kanisa la Ulimwengu, Makanisa ya Kikanda, Kitaifa, Kijimbo na sasa kuanza kuelekeza nguvu katika maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya Kiparokia. Lengo ni kuwawezesha watu wa Mungu kutembea kwa pamoja katika umoja kama Kanisa zima: kama sehemu ya mchakato wa uelewa wa Injili; kwa kusoma alama za nyakati na kuangalia mahitaji ya makundi maalum ndani ya Kanisa kama ilivyo wakati huu, Kanisa linapojiandaa kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu wa vijana, mwezi Oktoba 2018. Itakumbukwa kwamba, Sinodi hii inaongozwa na kauli mbiu: Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Kanisa pia limeadhimisha Sinoadi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, ili kuliwezesha Kanisa kusimama kidete kutangaza, kutetea na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa kuwakusanya watoto wa Mungu ili kuwa karibu zaidi kati yao; hatimaye, waweze kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Lengo ni kuweza kukabiliana na changamoto za shughuli za kichungaji, wakiwa wameungana kama Kanisa. Yote haya ni kutaka kuonesha umuhimu wa “Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baada ya maadhimisho ya Sinodi kwa ngazi la Kanisa la Kiulimwengu, Kikanda, Kitaifa, Kijimbo, kuna haja ya kuanza kujielekeza katika maadhimisho ya Sinodi za Kiparokia.

Sinodi hizi zitawasaidia waamini Parokiani kuchota utajiri wa amana na nyaraka mbali mbali zinazotolewa na Kanisa kwa ajili ya kuboresha maisha na utume wa maisha ya Kiparokia, katika Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo: Shule ya Neno, Sakramenti na Ukarimu mintarafu uhalisia wa maisha ya Parokia husika. Inaweza kuwa ni nafasi kwa Makanisa mahalia kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto za shughuli za kichungaji kwa umoja na mshikamano dhati. Kimsingi, “dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ndio mwelekeo mpya wa mchakato wa maisha na utume wa Kanisa!

Kumbe, Kanisa mahalia kuanzia sasa halina budi kuwekeza katika majiundo ya mihimili ya uinjilishaji itakayosaidia kumwilisha dhana hii katika uhalisia wa maisha ya Makanisa mahalia. Askofu Michael Msonganzila ametumia fursa hii, kumshukuru na kumpongeza Padre Afred Stanslaus Kwene kutoka Jimbo Katoliki la Musoma  aliyetetea kazi yake ya utafiti katika Shahada ya Uzamivu, kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, kilichoko mjini Roma, Jumatano, tarehe 13 Juni 2018.

Hili ni tukio ambalo limehudhuriwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na Askofu Michael Msonganzila aliyejitaabisha kuja Roma kushuhudia Padre wake akivitwa taji ya ushindi baada ya “patashika nguo kuchanika” kwa muda wa miaka mitano! Askofu Msonganzila amesikika akisema, Sinodi Musoma, inaanza upya, ili kuhakikisha kwamba, yale maamuzi yaliyofikiwa yanasaidia kuboresha maisha ya familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Musoma.

Kwa upande wake, Padre Afred Stanslaus Kwene aliyefanikiwa kutetea kazi yake na kufaulu kwa alama za juu, ameshukuru Mungu kwa neema, baraka na huruma yake katika hija ya maisha na wito wake. Anamshukuru na kumpongeza Askofu Michael Msonganzila kwa kwa kuonesha na kushuhudia moyo na karama ya ubaba. Padre Kwene ameahidi kuendelea kutangaza, kushuhudia na kutumia vyema matunda ya taaluma yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.