2018-06-07 10:22:00

Siku ya Kuombea Wongofu na Utakatifu wa Mapadre Duniani 2018


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 6 Juni 2018, amewakumbusha waamini kwamba, Ijumaa, tarehe 8 Juni 2018, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Juni wote umetengwa kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni wakati muafaka kwa waamini kusali, kuwaombea na kuwategemeza mapadre wao, ili waweze kuishi na kutenda kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya upendo wenye huruma!

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma, faraja na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni kisima cha neema, baraka na Sakramenti za Kanisa! Kwani, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa mkuki, humo ilitoka “Damu na Maji”, alama ya Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu; chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kunako Mwaka 2002, Mtakatifu Yohane Paulo II alianzisha Siku ya Kuombea Wongofu na Utakatifu wa Mapadre Duniani kwa kuwashirikisha waamini walei, ili kuwaombea na kuwasindikiza Mapadre wao kwa sala na sadaka zao. Siku hii inaadhimishwa sanjari na Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Ni mwaliko kwa Wakleri kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wake katika maisha na utume wao miongoni mwa familia ya Mungu.  Ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na utume huu, kuna haja kwa Mapadre kujifunza kuwa na moyo wa unyenyekevu, upole na uvumilivu, kwa kutambua kwamba, wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya watu katika mambo matakatifu. Padre ni mhudumu wa Sakramenti za Kanisa, Neno na huduma kwa familia ya Mungu. Anapaswa kukuza na kudumisha maisha na wito wake kwa njia ya sala, tafakari, Sakramenti za Kanisa pamoja na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Mapadre wajenge na kudumisha umoja na mshikamano na Maaskofu wao katika sala, tafakari, mafungo na maisha ya kawaida. Mapadre wamekirimiwa upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu, Kuhani mkuu wa Agano Jipya. Mapadre wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu wa mataifa, ili kuweza kuadhimisha Mafumbo ya Ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwawezesha kushiriki maisha ya uzima wa milele! Mapadre wakuze ndani mwao moyo wa huruma, msamaha na upatanisho wa kweli!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anasema, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la Wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4).  

Katika Sura ya tano Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kuhusu: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha ya kikristo ni mapambano endelevu yanayohitaji nguvu na ujasiri, ili kumpatia nafasi Kristo aweze kushinda na hatimaye, waamini kufurahia maisha. Waamini watambue kwamba, shetani, Ibilisi yupo na wala si dhana ya kufikirika tu! Waamini wawe macho na waendelee kukesha na kusali kwa kutambua kwamba, ushindi wao unafumbatwa katika Msalaba wa Kristo.

Utakatifu ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani. Huu ni mwaliko wa kupambana na “giza la maisha ya kiroho” kwa kujikita katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho kwa kutafakari kwa kina na mapana matamanio halali ya maisha, uchungu na fadhaa katika maisha yao; hofu na mashaka ili kutambua njia zinazowaelekeza katika uhuru wa kweli, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati kadiri ya mwanga wa Kristo Mfufuka. Mang’amuzi ya maisha ya kiroho, yawasaidie waamini kutambua Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Waamini wampatie nafasi Kristo Yesu ili aweze kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao! Furaha ya kweli anasema Mtakatifu Bonaventura imetundikwa kwenye mti wa Msalaba. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwaondolea woga na hofu zisizokuwa na mashiko ili kuanza mchakato wa kutoka katika ubinafsi, tayari kuliendea Fumbo la maisha ya Mungu, anayewasaidia waja wake kutekeleza utume wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya ndugu zao katika Kristo!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” kwa kumwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake wa kimama, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Wosia huu wa kitume utawasaidia waamini kuambata hija ya utakatifu wa maisha, ili kweli waweze kuwa ni watakatifu kwa ajili ya utukufu wa Mungu kwa kusaidiana na kuhimizana katika mchakato wa utakatifu wa maisha, ili waamini wote waweze kushiriki furaha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.