2018-06-05 15:38:00

Umoja wa Mataifa waiomba Serikali ya Kenya kulinda watetezi wa mazingira !


Serikali ya Kenya imeshauriwa kuchukua hatua za  haraka kulinda watetezi wa mazingira  ambao sasa wanakabiliwa na vitisho pamoja na udhalilishwaji. Watetezi hao wa masuala ya mazingira ni Alfred Ogola, Wilfred Kamencu, Anastancia Nambo na Kavumbi Munga. Hata hivyo taarifa inasadikika kuwa wamekuwa wanakabiliwa na vitisho baada ya kutoa ushahidi dhidi ya myeyushaji wa madini anayeshutumiwa kuharibu mazingira. Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yao 30 Mei 2018 huko Geneva, Uswisi wametaka vitisho dhidi ya watetezi hao vikome.

Taarifa zinazungumzia kuwepo kwa ugonjwa unaosababishwa na sumu ya risasi katika eneo la karibu na sehemu ya kiwanda hicho cha kuyeyusha risasi. Kesi ilifunguliwa na watetezi hao wakatoa ushahidi, na sasa wanapata vitisho. Mathalani watu wasiojulikana wamekuwa wakienda nyumbani kwa watetezi hao nyakati za usiku na kugonga milango yao huku wakiwapigia makelele wakiwataka wafungue. Mmoja wao alishambuliwa na kumwagiwa vitu ambavyo vilishababisha macho yake kuwashwa pamoja na kuvimba.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema, kamwe haikubaliki kwamba watu hao waendelee kutishwa, kushambuliwa na kufedheheshwa mara kwa mara na hakuna hata mtu mmoja ambaye amewajibishwa. Watu hao wanatarajiwa kutoa ushahidi mara nyingine  katika kesi  dhidi ya serikali na myeyushaji wa risasi kwa kukiuka haki dhidi ya  mazingira salama yaliyowekwa katika ibara 42 ya katiba ya Kenya. Hata hivyo taarifa kutoka vyombo vya Umoja wa Mataifa  inasema kuwa  ni kwa  mara ya  tatu wataalam wa Umoja wa Mataifa wakiiomba serikali ya Kenya kulinda na kuheshimu haki za wanamazingira na hadi sasa serikali ya Kenya haijatoa kauli yoyote.

Sr Angela Rwezaula 
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.