2018-06-04 13:57:00

Wadau wa tasnia ya habari zingatieni: pembezoni, ukweli na matumaini


Bwana Biagio Agnes ni kati ya waandishi wa habari mahiri nchini Italia, aliyesimama kidete kulinda na kudumisha huduma kwa umma, akiwataka wadau wa tasnia ya habari kujitahidi kutoa habari sahihi na za kweli; zinazoaminika na kutolewa kwa wakati! Hii ni changamoto kwa waandishi wa habari kuhakikisha kwamba, wanaendelea kujikita katika ukweli badala ya kutafuta masilahi yao binafsi au mashirika yao.

Haya yamesema na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Juni 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Biagio Agnes, kama sehemu ya utoaji wa tuzo ya kimataifa kwa wadau wa habari waliojipambanua kwa kuwajibika sanjari na kujikita katika weledi na taaluma ya mawasiliano ya jamii! Baba Mtakatifu amewakumbusha wadau katika tasnia ya mawasiliano kwamba, kazi yao ni muhimu sana katika mchakato wa majiundo ya watu, mwono na mwelekeo wao katika matukio mbali mbali ya maisha.

Tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa sasa inakabiliwa na mabadiliko makubwa kuelekea katika mfumo wa kidigitali pamoja na mageuzi yanayopaswa kufanywa kwenye vyombo husika kwa kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa waandishi wa habari kuandika habari zinazotoka pembezoni mwa jamii; pili ni kujikita katika ukweli na tatu na kuwajengea watu matumaini.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mara nyingi miji mikuu imekuwa ni kitovu cha habari, lakini, wadau wa mawasiliano hawana budi kukumbuka kwamba, hata watu wanaoishi pembezoni mwa jamii nao ni sehemu muhimu sana ya habari! Mara nyingi, hizi ni habari zinazogusa mateso na mahangaiko ya watu; athari za umaskini unaowatesa watu, lakini, wakati mwingine ni historia zinazofumbatwa katika mshikamano mkubwa, unaoweza kuwasaidia watu kuona ukweli wa dunia ambayo imepyaishwa!

Pili, Ukweli! Baba Mtakatifu anasema, mwandishi wa habari anapaswa kuandika kile anachofikiri kwa uelewa kamili pamoja na kuwajibika barabara katika tukio zima. Ni jambo la msingi sana, ikiwa kama, waandishi wa habari hawatambukia katika kishawishi cha kutafuta masilahi yao wenyewe au kwa ajili ya kukuza sera fulani katika jamii. Leo hii, mawasiliano yameboreka na yanasafiri kwa kasi kubwa, kiasi kwamba, wakati mwingine si rahisi sana kwa watu kupata nafasi ya kupembua ukweli wa mambo! Kumbe, ikionekana kuwa inafaa ni afadhali waandishi wa habari kukaa kimya, badala ya kumjeruhi mtu au kikundi cha watu au kufisha tukio fulani katika maisha. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hii changamoto si rahisi sana, kwani wakati mwingine historia ya maisha ya mtu inafahamika zaidi, mwishoni, mwaliko kwa waandishi wa habari kuwa na ujasiri na manabii katika taaluma yao!

Tatu, Matumaini! Baba Mtakatifu anakaza kusema, haiwezekani kutoa taarifa bila kugusia mateso na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia, vinginevyo, hii ingekuwa ni dunia ya kufirika. Hata katika kutangaza umaskini na hali ya kukata tamaa, lakini, pia waandishi wa habari hawana budi kupandikiza mbegu ya matumaini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wajumbe wa Mfuko wa wa Biagio Agnes kwa kuendeleza Jukwaa la Habari za Utafiti wa Kitabibu na Kisayansi badala ya mwelekeo wa sasa wa watu kujitafutia habari za tiba zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Baraza la Kipapa la Utamaduni hivi karibuni limehitimisha kongamano la kimataifa ambalo limejadili kwa kina na mapana tema hizi. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza wadau katika tasnia ya habari kuhakikisha kwamba, wanafanya majadiliano ya kisayansi na kijamii yanayojikita katika uwajibikaji na kuyapatia majina yao, bila kumung’unya mung’unya maneno. Waandishi wa habari wawe makini kutoa habari kamili na wala si kuchagua kadiri ya vionjo na mafao yao binafsi: kisiasa, kiuchumi au kisera.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.