2018-06-04 08:37:00

Papa Francisko: Fumbo la Ekaristi Takatifu livunjilie mbali ubinafsi!


Waamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili iliyopita, tarehe 3 Juni 2018, wameadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, “Corpus Domini”, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani ya Kanisa ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, yaani “Mwili na Damu yake Azizi”. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Kristo Msalabani na Agano la Upendo. Kila Jumapili, waamini wanakusanyika kusherehekea Sakramenti ya Sadaka ya Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Huku wakiwa wanavutwa na uwepo wake halisi katika maumbo ya Mkate na Divai, waamini wanamwabudu na kumtafakari kwa jicho la imani, Kristo Yesu aliyejificha katika maumbo ya Mkate na Divai, ambayo sasa yanakuwa ni Mwili na Damu yake Azizi.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Kila wakati waamini wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu wanapata mang’amuzi ya Agano Jipya, kilele cha umoja kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake. Waamini hata katika unyonge na umaskini wao, katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa historia anayotaka Mwenyezi Mungu. Ibada ya Misa Takatifu ni tukio la hadhara linalofanya rejea katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Waamini kwa kushiriki Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, wanakuwa ni sehemu ya Mwili wake, kwa kupokea upendo unaowawajibisha kujimega na kujitoa kwa ajili ya wengine! Hiki ndicho kiini cha Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Upendo, unaotolewa kwa ajili ya wengine. Waamini wanamtafakari Kristo Yesu, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, Mkate uliomegwa na Damu yake Azizi iliyomwagika kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Huu ni moto wa upendo unaounguza: ubinafsi; unaotakasa mtindo wa kutoa kile kidogo walichopokea na kuwasha ari na mwamko mpya, wa kutaka kujiunga na Kristo Yesu, Mkate uliomegwa na Damu iliyomwagika kwa ajili ya jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni Fumbo lenye mvuto kwa Kristo Yesu na linalowageuza waamini kuwa ni sehemu ya maisha yake. Ni shule ya upendo halisi; uvumilivu na sadaka kama Kristo Yesu, alivyofanya pale juu Msalabani. Waamini wanafundwa kuwa wakarimu kwa wale watu wanaohitaji kupendwa; msaada kwa wale wanaotafuta msaada; wajasiri kwa wale waliokata tamaa, wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wale wote wanaoogelea katika upweke hasi! Uwepo hai wa Kristo katika Ekaristi Takatifu ni sawa na Mlango wazi kati ya hekalu na barabara; kati ya imani na historia; kati ya mji wa Mungu na mji wa binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu, yanahitimisha maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwaka huu, anarejesha tena utamaduni na Mapokeo yaliyoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI hadi kufikia mwaka 1978 kwa kutembelea na kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu katika maeneo mbali mbali ya Jimbo kuu la Roma. Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wamefutalia na kushiriki maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kama sehemu ya ushiriki wao kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.