2018-05-30 10:41:00

Wanawake Wakatoliki wampongeza Papa Francisko kwa kuwajali!


Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, limemwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua ya wazi, kumshukuru na kumpongeza kwa uongozi imara na thabiti, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya watu wote wa Mungu. Lakini  zaidi linamshukuru kwa kuguswa na mahangaiko ya watu, changamoto na magumu wanayokabiliana nayo kila kukicha! Linampongeza kwa moyo wake wa: upendo, huruma na furaha inayomwilishwa katika imani na kwamba, wao kama wanawake Wakatoliki wanapenda kumuunga mkono yeye pamoja na viongozi wote wa Kanisa katika maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga ulimwengu unaojikita katika haki na maendeleo endelevu!

Wanawake Wakatoliki wanapenda kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuwashirikisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu ameonesha kuguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wanawake sehemu mbali mbali za dunia hasa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kumbe, ni wajibu wa wanawake pia kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kusaidiana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawawake wanapaswa kuhusishwa kikamilifu katika mchakato wa majadiliano, ili waweze kuchangia ustawi na mafao ya wengi, kwa kuwapatia wanawake nafasi ya kutumua karama na mapaji yao.

Wanawake Wakatoliki wanasema, umefika wakati wa kumwilishwa mawazo katika uhalisia wa maisha ya watu badala ya watu kuendelea “kuning’inia kwenye ombwe. Wanawake washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wanampongeza Baba Mtakatifu ambaye katika Wosia wake wa kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” anakazia umuhimu wa majadiliano katika maisha ya ndoa na familia ili kukuza na kudumisha upendo ndani ya familia. Majadiliano yajikite katika ukweli na uwazi; kwa kusali na kutafakari; kwa kukazia mambo msingi katika maisha, ili kukuza na kudumisha Injili ya familia. Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa majadiliano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu.

Katiba mpya ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha iliyopitishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Mei 2018 inabainisha kwamba, Baraza hili lina dhamana na wajibu wa kukuza na kudumisha wito, maisha na utume wa waamini walei katika Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Waamini walei ni sehemu muhimu sana ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanafanywa kuwa ni taifa la Mungu na hivyo kushirikishwa huduma ya kikuhani, kinabii na kifalme ya Kristo Yesu. Waamini walei wanatekeleza kadiri ya uwezo wao, utume wa taifa lote la Kikristo katika Kanisa na katika ulimwengu. Hawa ni waamini wanaoshiriki katika vyama na mashirika mbali mbali ya kitume ndani ya Kanisa.

Baraza litakuwa na dhamana na wajibu wa kuwasaidia waamini walei kuyafahamu Mafundisho tanzu ya Kanisa. Waamini walei wanao wajibu wa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini walei wanakumbushwa kwamba, uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na wale wote wanaoteseka ni furaha na matumaini, machungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Kumbe, waamini walei wanapaswa kujikita katika shughuli za uinjilishaji katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Baraza linawajibika pia kuwahamasisha waamini kujikita katika katekesi makini na endelevu; kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na Maisha ya Kisakramenti; matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kushiriki katika ustawi na maendeleo ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.