2018-05-29 15:49:00

Papa: husirudi nyuma katika mantiki za dunia,zinaondoa uhuru!


Katika kipindi cha majaribu, hakuna kurudi katika misimamo ya dunia hii inayotoa uhuru wa uongo, badala yake ni kubaki katika safari ya kuelekea utakatifu. Ndiyo ushauri wa Baba Mtakatifu Francisko alioutoa wakati wa mahubiri yake Jumanne tarehe 29 Mei 2018 katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican.  Katika mahubiri, ameongozwa na Somo la Kwanza la Mtakatifu Petro (1Pt 1,10-16) ambapo Petro anaalika wakristo kutembea katika utakatifu. Baba Mtakatifu anasema, huo   ni wito wa utakatifu ambao ndiyo wito wa Kanisa ili kuishi kama mkristo na ndiyo maana ya kusema kuishi utakatifu. 

Baba Mtakatifu amesema, mara nyingi sisi tuna fikiria utakatifu kama kitu cha kushangaza, kam vile kuwa na maono au kusali sala  iliyo kuu zaid, au wengine wanafikiri kuwa mtakatifu maana yake ni kuwa na sura ya sanamu. Hapana!  kuwa Mtakatifu ni jambo jingine. Ni kutembea katika njia ambayo Bwana anatufundisha. Je ni nini maana ya utakatifu? Baba Ntakatifu anasema kuwa  Mtakatifu Petro anatoa jibu ya kuwa: Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. 

Tembeeni katika utakatifu, ina maana ya kutembea kuelekea katika neema ambayo unakutana,wakati unaelekea kwenye matumaini, kuwa na nia ya kwenda kukutana na Kristo Yesu . Baba Mtakatifu anatoa mfano kwamba ni kama vile unapotembea kuelekea katika mwanga:;mara nyingi huoni barabara vizuri kwa sababu ya mwanga hafifu. Lakini huwezi kukosea barabara kwa sababu ya kuona mwanga mbele na unajua njia hiyo. Lakini wakati ukitembea ukiwa na  mwanga nyuma ya mabega utaona njia vizuri, lakini ki ukweli mbele kuna kivuli kwa sababu hakuna mwanga!

Ili kutembea kuelekea utakatifu ni lazima kuwa huru na kuhisi uhuru. Baba Mtakatifu ameonya: lakini pamoja na hayo kuna hatari nyingi za utumwa. Na ndiyo maama Petro anashauri kutokurudi nyuma katika shauku za wakati  ule mlipokuwa wajinga. Hata Mtakatifu Paulo katika Barua ya Warumi inasema: Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Baba Mtakatifu anasema kuwa ina maana kwamba usiingie katika taratibu za dunia hii. 

Hiyo ndiyo tafsiri safi ya ushauri wa kutofuata taratibu za ulimwangu, kwa maana ya kufikiria kiulimwengu, namna ya hukumu inayotolewa na dunia, kwasababu hali hiyo inatoa uhuru wa mtu. Ili kuelekea katika utakatifu, ni lazima uwe huru; uhuru wa kwenda ukitazama mwanga na kwenda mbele, kwa sababu tunaporudi nyuma kama asemavyo mtakatifu, namna ya kuishi kama mwanzo kabla ya kukutana na Yesu Kristo au kurudi katika taratibu za dunia hii ndiyo maana ya kupoteza uhuru.

Katika kitabu cha Kutoka, kinaonesha kwa dhati jinsi gani watu wa Mungu mara nyingi walitaka kutazama mbele kuelekea katika wokovu, lakini walikuwa wakirudi nyuma. Walilalamika na walikuwa wakifikiria maisha mazuri waliyopata huko Misri, wakila vitunguu na nyama. Katika kipindi cha matatizo, watu hurudi nyuma, na kupoteza huru: ni kweli walikuwa wanakula mambo mazuri lakini katika meza ya utumwa.

Katika kipindi cha majaribu daima kuna kishawishi cha kutaka kutazama nyuma, kutazama mipango ya ulimwengu na mipango ambayo ilikuwa inafanyika kabla ya kuanza safari ya wokovu, lakini bila kuwa huru. Bila kuwa na huru hakuna utakatifu baba Mtakatifu amethibitisha. Uhuru ni hali inayo kuruhusu kuweza kutambea ukitazama mwanga mbele. Usiingie katika taratibu za kiulimwengiu, badala yake utazame mbele, utazame mwanga ambao ndiyo ahadi na ndiyo matumaini.

Hiyo ndiyo ahadi aliyo watolea watu wake katika jangwa. Walipokuwa wakatazama mbele walikwenda vizuri, lakini mara walipokuwa wakianza kukumbuka yaliyo pita, kwasababu ya kutokula mambo mazuri waliyo kuwa wanapewa pale, wajisahau kuwa pale walikuwa huru na wala siyo watumwa tena.  Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amehitimisha akirudia kusema: Bwana anaita kila siku katika utakatifu! 

Pamoja na hayo kuna hata vipimo viwili vya kujua kama kweli unaelekea katika utakatifu. Hawali ya yote kama tunatazama kuelekea katika mwanga wa Bwana na matumainiili uweze kumpata; pia  tunapokumbwa na majaribu, tunatazama mbele bila kupoteza uhuru kamili  wa kukimbilia katika mipango ya kidunia ambayo inatoa ahadi za uongo. Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni matakatifu, ndiyo amri ya Bwana! Baba Mtakatifu anakumbusha tena, kuomba Bwana wote neema ya kutambua vema nini maana ya safari ya utakatifu na njia ya uhuru, lakini kwa matumaini ya kwenda kukutana na Yesu. Halikadhalika kutambua nini maana ya kwanda kukutana na taratibu za kidunia ambazo tuliiziishi wote kabla ya kukutana na Yesu!

 Na Sr Angela Rwezaula
 Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.