2018-05-29 08:04:00

Majadiliano ni nyenzo msingi katika kukabiliana na changamoto mamboleo


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol amekuwepo mjini Roma kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ambayo yameongozwa na kauli mbiu “Sera na mtindo mpya wa maisha katika kipindi cha digitali”. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa na ameshiriki katika kuchangia mada kwa kukazia “Mafao ya wengi kama ajenda ya pamoja kwa Wakristo wote.”

Kwa namna ya pekee, Patriaki Bartolomeo wa kwanza, katika uchambuzi wake amejikita katika sekta ya uchumi na ekolojia; Sayansi na teknolojia; jamii na siasa. Mshikamano na mafungamano ya kiekumene ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko; chemchemi ya furaha ya Injili na wokovu kwa walimwengu. Tunu msingi za Kiinjili hazina budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kijamii kwa kuongozwa na mambo yafuatayo: utu na heshima ya binadamu; mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hizi ni kanuni msingi zinazoweza kutumiwa na Kanisa ili kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Familia ya Mungu haina budi kujenga utandawazi na utamaduni wa mshikamano ambao kwa sasa unaonekana kutoweka kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Patriaki Bartolomeo wa kwanza, hivi karibuni akitoa hotuba yake kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Bwana Gerardo Angel Bugallo Ottone, Balozi wa Hispania mjini Vatican, amekazia umuhimu wa Makanisa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene, kidini, kitamaduni kati ya jamii pamoja na watu wa Mataifa.

Anakaza kusema, katika maisha na utume wake, anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa majadiliano kama msingi wa mahusiano na mafungamano kati ya watu. Hii inatokana na ukweli kwamba, ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto pevu zinazofumbatwa katika: misimamo mikali ya kidini na kiimani; sera na mikakati ya uchumi inayotafuta faida kubwa na dini ambazo utu na heshima ya binadamu si mali kitu! Majadiliano ndiyo njia pekee, inayoweza kurejesha utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na mchakato wa ujenzi wa uchumi shirikishi.

Kanisa ambalo ni aminifu kwa Kristo Yesu ni shuhuda wa makini wa historia inayopambwa na: Watakatifu pamoja na Mababa wa Kanisa waliotambua na kumwilisha Amri ya upendo kwa Mungu na jirani, daima wakaendelea kujikita katika majadiliano, hata katika nyakati za giza katika maisha na utume wa Kanisa; pale ambapo misimamo mikali ya kiimani, ilionekana kana kwamba, inataka kutawala. Kanisa hata leo hii, linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wakristo wajenge umoja na mshikamano wa dhati ili kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wakristo wakiwa wameshikamana wanaweza kukabiliana kwa dhati kabisa na changamoto za haki jamii; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; ukosefu wa haki na amani duniani; pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, dhana ya majadiliano ni jibu muafaka kwa changamoto mbali mbali zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Anatambua fika matatizo na changamoto katika majadiliano, lakini yote haya yanapaswa kuangaliwa kama kichocheo cha kusonga mbele na wala si kikwazo cha umoja na mshikamano kati ya Makanisa. Katika mchakato wa majadiliano, Kanisa la Kiorthodox linapenda kujiaminisha chini ya ulinzi na uongozi wa Roho Mtakatifu na neema ya Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu, ambaye katika Sala yake ya Kikuhani, amewaombea wafuasi wake ili wawe wamoja! Mwishoni mwa hotuba yake, amewatakia wote: amani, ustawi na maendeleo ya kweli: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.