2018-05-29 13:30:00

Kanisa litaendelea kujizatiti kutetea Injili ya uhai!


Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika mtu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu ni asili na kikomo cha maisha ya mwanadamu. Hakuna mazingira yoyote yale yanayoweza kujitwalia haki na mamlaka ya kuharibu zawadi ya uhai. Mama Kanisa anafundisha na kukazia kwamba, uhai wa binadamu sharti uheshimiwe na ulindwe na kwamba, uhai ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Leo hii kuna wimbi kubwa la utamaduni wa kifo unaoendelea kuwanyemelea watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Sheria-Kanuni maadili, utu wema; uhuru na dhamiri nyofu ni kati ya mambo msingi ambayo yamedadavuliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, 28 Mei 2018 alipokuwa anazungumza na Shirikisho la Madaktari Wakatoliki Duniani, FIAMC. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Majiundo ya madaktari, kimsingi yanajikita katika: maisha ya kiroho, kiutu na maadili ya kibaiolojia.

Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wake wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya Binadamu.” Uliochapishwa kunako tarehe 25 Julai 1968 unakazia dhamana ya kurithisha uhai wa binadamu na kwamba wazazi wakiwa huru wanawajibika kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji na malezi. Kumbe,  kuna haja kwa familia ya Mungu, lakini zaidi wale wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanajikita katika utakatifu wa maisha ya binadamu, taaluma na weledi wa madaktari katika kudumisha uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Ireland hivi karibuni imepiga kura ya maoni na kufanikiwa kubadilisha kifungu cha katiba kilichokuwa kinazua tabia ya utoaji mimba kisheria. Utamaduni wa kifo umeshinda na kwamba, hivi karibuni, sheria inayoruhusu utoaji mimba itatungwa na kuanza kutekelezwa mara moja! Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha anasema, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha zawadi ya maisha, kwani daima ni maafa na kilio, pale maisha ya binadamu yanapoyoyoma! Kanisa linawahamasisha watoto wake kuwa ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akina mama wanaothubutu kuchukua mimba, kujifungua, kulea na kuwatunza watoto wao hawa ni mashuhuda wa Injili ya uhai; kwa sababu ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wao.

Askofu mkuu Paglia anasikitika kusema, leo hii maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu yanatumiwa na baadhi ya wataalam dhidi ya zawadi ya maisha, inayopaswa kulindwa, kusindikizwa na kuendelezwa. Ubinafsi na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko ni mambo yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika utamaduni wa kifo; kwa kupoka haki msingi za binadamu dhidi ya watoto ambao walipaswa kuzaliwa. Kutokana na changamoto hizi, kuna haja kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha maisha ya binadamu katika hatua zake mbali mbali!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, familia bado inaendelea kuwa ni kitovu cha Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu! Ni wajibu wao kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu!

Familia kadiri ya mpango wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu na familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia! Siku ya IX ya Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 22- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Maandalizi haya yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland limesikitishwa sana na matokeo ya kura ya maoni ambayo kwa sasa utoaji mimba unaruhusiwa kisheria: Huu ni wakati kwa Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na familia kwa vitendo, ili kuonesha ule upendo na msamaha wa Kristo Yesu kwa familia ya binadamu. Kanisa halina budi kuwa karibu zaidi na wanawake wanaokabiliana na changamoto za maisha, ili kuwasaidia kwa kuondokana na kishawishi cha kutaka kumezwa na utamaduni wa kifo.

Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Dublin anasema, leo hii kuna wanawake wengi wanaokabiliwa na umaskini wa hali, kipato pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Hawana uhakika wa makazi bora na salama kwa ajili yao binafsi na watoto wao; watu wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kiasi hata cha kutafuta njia za mkato katika maisha! Ireland katika miaka ya hivi karibuni, imejikuta ikitumbukia katika ombwe kubwa la utupu na mtikisiko wa kanuni maadili na utu wema; kwa kuridhia ndoa za watu wa jinsia moja pamoja na talaka za chapuchapu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.