2018-05-29 16:20:00

Kalenda ya Shughuli za Baba Mtakatifu Francisko mwezi Juni-Agosti 2018


Shirika la Habari za Vatican limetoa ratiba elekezi ya shughuli za kichungaji, kama vile ziara, mikutano na maadhimisho ya Baba Mtakatifu kwa miezi ya kiangazi yaani: (Juni, Julai na Agosti). Kwa mujibu wa kalenda, tarehe 3 Juni 2018, ni Sikukuu ya Mwili na Damu ya Yesu ambapo Baba Mtakatifu Francisko atakuwa Ostia Roma, saa 12.00 Jioni saa za Ulaya kuadhimisha Misa Takatifu, katika Kanisa la Mtakatifu Monica na kuafuatia maandamano ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo hadi katika Kanisa la Mama Yetu wa Bonaria na kuhitimishwa na baraka ya Ekaristi Takatifu.

Tarehe 21 Juni Baba Mtakatifu Francisko atafanya ziara yake ya kiekumene huko Geneva na tarehe 28 Juni 2018, kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya ataadhimisha Mkutano wa Makardinali na kuwasimika Makardinali wapya 14 kutoka katika Mabara matano. Tarehe 29 Juni ni Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, ambapo katika Uwanja wa Mtakatifu Petro saa 3.30 ,asubuhi masaa ya Ulaya Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada Takatifu ya Misa na mwisho kubariki Palio Takatifu kwa ajili ya Maaskofu wakuu wapya walioteuliwa hivi karibuni kutoka sehemu mbali mbali za dunia

Katika mwezi wa Julai, 2018, unafunguliwa na  siku ya Jumamosi ya tarehe 7 kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko  katika mkutano wa kiekumene na sala kwa ajili ya kuombea amani ya nchi za Mashariki, huko Bari kusini mwa Italia. Na mwisho mwezi wa Agosti , tarehe 25 na 26 Agosti,itakuwa ni  Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu katika mji wa Dublin, Ireland kwenye Mkutano Familia Duniani. 

Na sr Angela Rwezaula 
Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.