2018-05-26 16:39:00

Papa Francisko anaenzi Ijumaa ya huruma ya Mungu kwa matendo!


Ijumaa ya Huruma ya Mungu ni siku maalum iliyotengwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu kuwa ni siku ya kuonesha kwa vitendo, matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia kama alama ya mwendelezo wa Mwaka wa Huruma ya Mungu.

Ijumaa, 25 Mei 2018, Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya, alitembelea Kituo cha Elimu cha “Elisa Scala” kilichoko nje kidogo ya mji wa Roma, ili kuwatembelea na kuzungumza na wanafunzi pamoja na walezi wao. Alipowasili Kituoni hapo, alilakiwa na Professa Claudia Gentili pamoja na umati wa wanafunzi uliokuwepo kituoni hapo. Shule hii, imepewa jina la “Elisa Scala” kama kumbu kumbu endelevu ya Mtoto Elisa aliyefariki dunia kunako mwaka 2015 kutokana na ugonjwa wa Saratani ya damu, akiwa na umri wa miaka kumi na mmoja.

Hata katika udogo wake, ni mtoto aliyekuwa na upendo mkuu kwa wazazi wake na kwa hakika alipenda sana kusoma. Baada ya mtoto Elisa kutupa mkono dunia, wazazi wake wakamua kuanzisha mradi huu kama njia ya kutekeleza ndoto ya mtoto wao aliyependa kusoma. Leo hii, kituo hiki kina Maktaba kubwa ya Elisa ambayo imechangiwa vitabu na wasamaria wema kutoka ndani na nje ya Italia. Akiwa kituoni hapo, Baba Mtakatifu Francisko amebahatika kukutana na kuzungumza na wazazi wa Marehemu Elisa; ametembelea Maktaba pamoja na kupata nafasi ya kukaa kwa muda na wanafunzi wanaosoma kituoni hapo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.