2018-05-25 14:26:00

Papa Francisko: Familia ni kitovu cha faraja, imani na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 25 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wa raia, wafanyakazi katika Idara ya Afya pamoja na familia zao. Imekuwa ni nafasi pia kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na waathirika wa vitendo vya kigaidi. Wote hawa amewashukuru kwa huduma makini kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Kanisa katika ujumla wake. Amewataka wafanyakazi wote hawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha kwa familia zao kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, familia ni jumuiya ya kwanza ambamo mtu anajifunza kupenda na kupendwa; mahali pa kufunza na kurithisha imani pamoja na kutenda mema. Familia imara na thabiti ni nguzo madhubuti kwa jamii na Kanisa kama sehemu muhimu sana ya kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuka kila kukicha! Katika magumu na machungu ya maisha; katika kinzani na mipasuko ya kijamii, familia inakuwa ni mahali pa kwanza kuonja changamoto zote hizi, kama chemchemi ya maisha na upendo. Familia inaweza kusaidia kuvuka changamoto zote hizi kwa amani na utulivu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, familia ya binadamu tangu hata katika simulizi za Maandiko Mtakatifu imekumbana na mauaji, kinzani na mipasuko ya kifamilia; maafa na mateso makali, kama ilivyokuwa hata kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Bikira Maria aliyatafakari na kuyahifadhi yote haya katika sakafu ya moyo wake! Wakati huo huo, Yesu alishuhudia, akasikiliza, akafurahi na kuteseka na wale wote aliokutana nao katika hija ya maisha na utume wake. Hawa ndio wagonjwa waliokuwa hawawezi kitandani; watu waliokuwa wanawaombolezea ndugu na watoto wao waliokuwa wamefariki dunia! Yesu alijichanganya na watu wote hawa na hivyo kuwa ni kiini cha faraja, imani na matumaini mapya! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mama Kanisa katika hija ya maisha yake ya kila siku anatambua uchungu na fadhaa; kinzani na mipasuko; hali ngumu ya kiuchumi, ukosefu wa fursa za ajira; mambo ambayo yanajionesha katika Injili. Kanisa ambalo linaongozwa na Roho Mtakatifu linataka kuwasindikiza wanafamilia katika hija ya maisha yake kwa kuwaonesha hatima ya maisha yao kwamba uchungu na kifo, havina nafasi ya mwisho katika maisha yao.

Kristo Yesu daima yuko kati pamoja na watu wake; anawaongoza na kuwasindikiza kwa huruma na kuwatakatifuza kwa upendo. Uwepo wake ni ishara ya huruma na upendo wa wazazi kwa watoto wao. Familia ni kitovu cha imani, mahali ambapo watu hujifunza kusali, kutumainia; kukuza na kudumisha tunu msingi za kifamilia kama chemchemi ya upendo na faraja ili kujenga na kudumisha amani; kwa kushikamana na kusaidiana, huku wote wakitambua madhaifu na mapungufu ya maisha yao! Ulimwengu mamboleo anasema Baba Mtakatifu Francisko, umesheheni changamoto nyingi ambazo askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wa raia wanakumbana nazo hata katika mji kama wa Roma. Mang’amuzi na tunu msingi za maisha ya kifamilia, zinawawezesha kuwa na uwiano, hekima na tunu msingi ambazo wanaweza kuzitumia kama rejea katika shughuli zao. Familia bora ina uwezo wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kijamii; ina uwezo wa kuwaelimisha watoto wake, ili wajisikie kuwa ni sehemu muhimu ya jamii, ili hatimaye: waweze kufikiri na kutenda kama raia wema, wanyofu na wakweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.