2018-05-25 16:25:00

Mwenyeheri Sr. Leonella ni shuhuda wa udugu, upendo na msamaha


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 26 Mei 2018 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anamtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Leonella Sgorbati kuwa Mwenyeheri. Ibada hii inaadhimishwa huko Piacenza, Kaskazini mwa Italia. Rosa Sgorbati alizaliwa tarehe 9 Desemba 1940 huko Piacenza na baadaye, akajiunga na Watawa Wamisionari wa Consolata na kupewa Leonella kama jina la kitawa.

Sr. Leonella alitumwa na Shirika lake nchini Kenya na hatimaye Somalia ili kuanzisha Chuo cha Wauguzi, Kaskazini mwa Mji wa Mogadisho, nchini Somalia. Huko ndiko alikouwawa kikatili kutoka na chuki za kidini. Kanisa linatambua ushuhuda wake wa imani, kama mtawa aliyesimama kidete kulinda na kutetea Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; ni shuhuda na chombo cha udugu, upendo na msamaha. Katika moyo wa unyenyekevu na huduma makini kwa maskini, Sr. Leonella aliweza kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo kwa ajili ya Mungu na jirani; na kwa hakika, alijitoa kimaso maso kama mbegu ya furaha ya Injili.

Kardinali Amato anasema, Sr. Leonella aliuwawa kikatili kunako tarehe 17 Septemba 2006 na kikundi cha waamini wa dini ya Kiislam waliokuwa na msimamo mkali wa kidini na kiimani. Wakati, alipokuwa anakaribia kukata roho, aliwaombea wauwaji wake msamaha, kwa sababu walikuwa hawajui watendalo. Huu ni ushuhuda wa Kikristo unaofumbatwa katika upendo, kwa kufuata Amri na Maagizo ya Kristo, kwa kusamahe bila kuchoka; kwa kusali na kuwaombea hata watesi wao, kielelezo makini cha Amri Mpya ya Upendo kadiri ya kipimo cha Kristo mwenyewe.

Kifodini cha Sr. Leonella Sgorbarti kimekuwa ni mbegu ya matumaini yatakayozaa matunda kwa wakati wake. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na dhana ya vita, chuki na uhasama, ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kununulia silaha, igeuzwe na kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Somalia wanaoendelea kuteseka kwa vita, magonjwa, ujinga na njaa.

Kardinali Angelo Amato anasema, kifodini cha Sr. Leonella ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo yanayojikita katika ukarimu, upendo na msamaha wa kweli. Huu ni mwaliko wa kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa. Waconsolata wanakumbushwa kwamba, licha ya nadhiri ya ufukara, usafi wa moyo na utii, kuna nadhiri ya nne ni sadaka, kiasi hata cha kuweza kumimina maisha kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Sr. Leonella ameweza kuishi kwa ukamilifu  Fumbo la Mateso ya Kristo, kama mfuasi amini, aliyejitahidi kumtafuta Mwenyezi Mungu, ili kutimiza mapenzi yake. Akajisadaka na kuonesha utii; unyenyekevu na unyofu wa moyo, ili kupandikiza mbegu ya upatanisho katika akili na nyoyo za watu. Ni mtawa aliyebahatika kutekeleza dhamana na majukumu yake katika hali ya ukimya pamoja na kushiriki suluba za maisha ya kila siku pamoja na ndugu zake katika Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.