2018-05-25 11:30:00

Familia ya Mungu nchini Msumbiji ina kiu ya haki, amani na maridhiano


Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linasema kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa haki, amani na maridhiano miongoni mwa familia ya Mungu nchini Msumbiji, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kikolezo muhimu sana cha maendeleo endelevu ya binadamu! Kifo cha Mwanasiasa mashuhuri na mpinzani mkuu wa Serikali ya FRELIMO Bwana Afonso Dhlakama, aliyefariki dunia hapo tarehe 3 Mei 2018, akiwa na umri wa miaka 65, kisiwe ni sababu ya kukwamisha mchakato wa majadiliano ya amani kati ya Rais Filipe Nyusi wa Msumbuji na Chama cha RENAMO ambayo tayari yalikuwa yanaendelea na kuanza kuonesha matumaini ya amani kwa familia ya Mungu nchini Msumbiji!

Askofu Joao Carlos Hatoa Nunes wa Jimbo Katoliki la Chimoio ambaye pia ni msemaji mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji anakaza kusema, mafanikio yaliyokuwa yamefikiwa kati ya Serikali na Chama cha upinzani cha RENAMO yaendelezwe. Kati ya  mambo yaliyokuwa yamefikiwa ni pamoja na uteuzi wa wakuu wa majimbo, ugawaji wa madaraka pamoja na kuhakikisha kwamba, wapiganaji wa RENAMO wanaingizwa katika vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Inasikitisha kuona kwamba, Hayati Afonso Dhlakama amefariki dunia, akiacha utupu katika uongozi wa RENAMO. Kwa wakati huu, RENAMO imemteu Bwana Ossufo Momade kushikilia madaraka hadi pale mkutano mkuu wa Chama cha RENAMO utakapofanya uchaguzi wake mkuu. Wachunguzi wa mambo wanasema, ari na moyo wa Mkataba wa Amani wa Roma uliotiwa sahihi kunako mwaka 1992 na hivyo kuweka msingi wa amani na maridhiano nchini Msumbiji, unapaswa kufufuliwa na kupyaishwa zaidi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Msumbiji.

Hakuna sababu tena kwa wananchi kurudi kwenye vita ya msituni kwani wamechoka na sasa wanataka maendeleo endelevu, yatakayozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika salam zake za rambi rambi wakati wa mazishi ya Bwana Afonso Dhlakama, Rais Filipe Nyusi alisema, Serikali yake inapania kujenga na kudumisha amani na maendeleo kwa wananchi wote wa Msumbiji bila kujali tofauti za itikadi zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.