2018-05-22 07:43:00

Papa Francisko aridhia maadhimisho ya Baraza kuu Australia!


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uamuzi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Australia kuadhimisha Baraza kuu litakalowahusisha wawakilishi wa familia ya Mungu nchini Australia ili kujadili kwa pamoja maisha, utume na changamoto zinazolikabili Kanisa nchini Australia kwa wakati huu. Hili ni tukio la kihistoria kuwahi kufanyika nchini humo, kwani historia inaonesha kwamba, kwa mara ya mwisho baraza kama hili lilifanyika yapata miaka 80 iliyopita!

Tangu wakati huo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuangaliwa katika mwanga wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mchakato wa kusikilizana na kujadiliana, umeanza rasmi wakati wa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2018. Kanisa linataka kujikita katika mchakato wa utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa dhati kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Ni wakati wa kusikiliza shuhuda za Imani, matumaini na mapendo; hali ya kukata tamaa na udhaifu wa binadamu, ili kuanza tena upya kwa nguvu, ari na moyo mkuu

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linawaomba watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu kwa njia ya sala, ili kuhakikisha kwamba, mkutano huu unafanikiwa, ili kujenga utamaduni wa kusoma alama za nyakati, kumsikiliza Mwenyezi Mungu pamoja na familia ya Mungu kusikilizana wao kwa wao, ili katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, waweze kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji utakaojibu kilio na matamanio ya watu wa Mungu nchini Australia kwa sasa na kwa siku za usoni! Waamini wanaweza pia kushirikisha mawazo yao kwa njia ya mitandao ya kijamii yatakayoratibiwa na hatimaye, kuwasilishwa kwenye mkutano wenyewe.

Askofu mkuu Timothy Costelloe, Mwenyekiti wa Baraza hili anasema, Kanisa lina matumaini makubwa kwamba, mkutano huu utasaidia kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya familia ya Mungu nchini Australia kuzungumza katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana katika unyenyekevu ili hatimaye, kwa pamoja waweze kusoma alama za nyakati na kujibu kilio cha familia ya Mungu nchini Australia: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watapewa kipaumbele cha kwanza ili kutoa maoni yao, jambo ambalo limewagusa watu wengi wakati wa mikutano elekezo kwa ajili ya tukio hili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.