2018-05-22 13:30:00

Kumbu kumbu ya miaka 40 tangu sheria ya utoaji mimba ipitishwe Italia


 Bwana Giovanni Paolo Ramonda, Rais wa Jumuiya ya Papa Yohane wa XXIII anasema, mwaka 2018, familia ya Mungu nchini Italia inafanya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Bunge la Italia lilipopitisha Sheria namba 194 inayoruhusu vitendo vya utoaji mimba. Ni sheria iliyopitishwa kwa kisingizio cha kutaka kuwapatia wanawake uhuru zaidi juu ya hatima ya maisha na afya zao. Lakini, kimsingi familia ya Mungu nchini Italia, imejikuta ikikumbatia utamaduni wa kifo na matokeo yake ndiyo hayo yanayoonekana sasa kwa kupungua kwa kiasi kikubwa cha watoto wanaozaliwa nchini Italia.

Don Benzi, muasisi wa Jumuiya hii aliwahi kusema, sera inayokumbatia utoaji mimba daima imekuwa na madhara makubwa kwa wanawake na watoto ambao wanaendelea kupoteza maisha kila kukicha. Matumizi ya vizuia mimba yamekuwa pia athari kubwa kwa wasichana na vijana wa kizazi kipya. Bwana Giovanni Paolo Ramonda anasema, vijana wa kizazi kipya nchini Italia wanapaswa kusaidiwa kuheshimu na kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kusababisha madhara makubwa. Vijana wawezeshwe kiuchumi, ili waweze kumudu changamoto za maisha ya ndoa na familia. Ushuhuda unaonesha kwamba, watoto waliosalimika kutoka kwenye mikono ya watu wakatili, wamekuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa jirani zao. Kumbe, Injili ya uhai ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.