2018-05-22 10:30:00

Hofu kuu ni: Miito, Ufukara wa Kiinjili na Wingi wa Majimbo, Italia


Bikira Maria alishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kama Mama wa Mkombozi. Alishiriki katika maisha ya hadhara ya Kristo Yesu hadi siku ile alipomwona Mwanaye wa pekee, akiinama kichwa na kukata roho pale Msalabani. Akakubali kupokea upendo wa Sadaka ya mateso na kifo chake Msalabani, alipokabidhiwa kwa Yohane, Mwanafunzi aliyempenda kwa kusema, “Mama, tazama mwanao”. Bikira Maria aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, aliendelea kusali pamoja na Mitume wa Yesu, huku wakisubiri Roho Mtakatifu aweze kuwashukia.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakakiri kwamba, Kristo Yesu ni mpatanishi wa pekee na Bikira Maria, aliyeshiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi na kwamba, ni mwombezi kwa ajili ya wokovu wa watu. Bikira Maria na Mama; ni mfano wa utimilifu wa Kanisa linalopaswa kuuiga utakatifu wa Mama wa Mungu, upendo wa kimama unaowawezesha watu kuzaliwa upya. Bikira Maria ni ishara ya tumaini thabiti na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri hapa duniani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufungua mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Jumatatu, tarehe 21 mei 2018 amesema, kwa hakika, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa, anayewafanya viongozi wa Kanisa kusikia na kutambua uwepo wake kati yao, wanapokutana kujadiliana masuala msingi katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini wataendelea kutambua na kuthamini: Ibada kwa Bikira Maria na Umama wa Kanisa. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amewaambia Maaskofu kwamba, kuna mambo makuu matatu yanayomkera sana moyoni mwake. Mosi: ni kuteteleka kwa miito mitakatifu ndani ya Kanisa; ukosefu wa ufukara wa kiinjili na uwazi katika matumizi ya rasilimali ya Kanisa inayopaswa kutumika kama kikolezo cha mchakato wa uinjilishaji na tatu ni kupunguza utitili wa majimbo kwa kuunganisha baadhi yao!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, takwimu zilizotolewa hivi karibu na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linaonesha kwamba, idadi ya miito ya maisha ya kipadre na kitawa nchini Italia inaendelea kupungua kila kukicha. Haya ni matokeo ya sumu ya uchoyo na ubinafsi; athari za utamaduni unaokumbatia mambo mpito; uchu wa mali na madaraka pamoja na kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ambazo zimepelekea hata kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia.

Kumekuwepo na kashfa ambazo zimelikumba Kanisa kiasi hata cha kuacha kurasa chungu katika maisha na utume wa Kanisa, hali ambayo pia imechafua ushuhuda wa Kanisa. Baba Mtakatifu kwa masikitiko makubwa anaendelea kujiuliza, Je, ni seminari na nyumba ngapi za malezi zitafungwa katika miaka ya hivi karibuni? Je, ni Makanisa na Makonventi mangapi yatafungwa kwa kukosa miito? Inasikitisha kuona nchi kama Italia ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ikizama katika ukame na uhaba wa miito. Huu ndio wakati wa kutafakari na hatimaye, kufanya maamuzi machungu kwa ajili ya kuhamasisha miito mitakatifu nchini Italia.

Jambo la kwanza linaloweza kufanyiwa kazi ili kukabiliana na uhaba wa miito ya mihimili ya Injili ni kwa majimbo nchini Italia kujenga na kudumisha utamaduni wa kubadilishana mapadre zawadi ya imani “Fidei Donum”. Kaskazini mwa Italia kuna uhaba mkubwa wa miito wakati ambapo Kusini mwa Italia, bado kuna dalili za vijana kutaka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wasi wasi wake wa pili unajikita katika ukosefu wa ufukara wa kiinjili na uwazi katika matumizi ya rasilimali ya Kanisa inayopaswa kuelekezwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima! Ufukara wa Kiinjili ni kinga na silaha madhubuti katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa shughuli za kitume na kichungaji sanjari na huduma makini kwa familia ya Mungu. Inasikitisha kuona kwamba, leo hii, kuna viongozi wa Kanisa ambao wanaelemewa sana na uchu wa mali na madaraka kiasi hata cha kupenda anasa na malimwengu, kashfa kubwa dhidi ya ushuhuda wa ufukara katika maisha na utume wa Kanisa.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wakleri na majimbo yamejikuta yakitumbukia katika kashfa ya wizi na ufisadi wa mali ya Kanisa! Kuna baadhi ya viongozi wametumia vibaya sana mali ya Kanisa na kushindwa kuwa waaminifu hata kwa senti kidogo zinazotolewa na “wajane” ndani ya Kanisa! Hapa kuna haja ya kusimamia, kutumia na kuratibu mali ya Kanisa kadiri ya sheria kanuni, maadili na utu wema. Viongozi wa Kanisa wasitumie fedha za Kanisa kufanya “matanuzi” kwa kupenda anasa na tafrija, watambue kwamba, wanawajibika mbele ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kulipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ambalo kwa miaka ya hivi karibuni, limeamua kuwekeza zaidi katika ufukara wa Kiinjili unaofumbatwa katika ukweli na uwazi wa matumizi ya rasilimali fedha ya Kanisa. Mchakato huu hauna budi kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kupunguza utitili wa majimbo kwa kuunganisha baadhi ya majimbo, changamoto ambayo ni kubwa na inaendelea kukabiliana na upinzani kutoka ndani na nje ya majimbo yenyewe! Lakini, ukweli wa mambo anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kuunganisha mjimbo nchini Italia, ili kukuza na kudumisha ufanisi katika maisha na utume wa Kanisa. Changamoto hii ni hitaji msingi la shughuli za kichungaji nchini Italia. Mwenyeheri Paulo VI katika maisha na utume wake, alikwisha kuiona changamoto hii, mara baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, sasa umefika wakati wa kuangalia tena mipaka ya Majimbo Katoliki nchini Italia; kwa kuzingatia idadi ya waamini; idadi ya mihimili ya uinjilishaji pamoja na rasilimali fedha, ili kuyawezesha majimbo kuweza kutekeleza shughuli zake za kitume na kichungaji kwa tija na ufanisi mkubwa. Changamoto hii inafanyiwa kazi pia na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu na baadaye, taarifa yake itawasilishwa kwenye Sekretarieti kuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa ajili ya maamuzi na utekelezaji wake. Umefika wakati wa kuanza utekelezaji wake bila kuchelewa anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.