2018-05-18 15:35:00

Pentekoste ni nafasi ya kumtafakari Roho Mtakatifu!


Utangulizi: “Na wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakasema matendo makuu ya Mungu Aleluya” karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu leo ikiwa ni sherehe ya Pentekoste. Siku hamsini baada ya ufufuko Yesu anaitimiza ahadi aliyowapa Mitume, ahadi ya kuwatumia Roho Mtakatifu, Roho atokaye kwa Baba na kwa Mwana, awaimarishe na awape nguvu ya kuuanza utume wao. Leo tunatafakari juu ya kiri ya imani juu ya Roho Mtakatifu na nafasi yake katika Kanisa, katika utume, katika maisha ya kila mmoja wetu na katika mpango wa Mungu wa wokovu kwa ulimwengu.

Masomo kwa ufupi: Somo la Kwanza (Mdo. 2:1-11) linaelezea tukio la siku ya Pentekoste. Pentekoste ya wayahudi ilikuwa ni sherehe ya mavuno ya kwanza ambayo waliisherekea siku hamsini baada ya pasaka yao iliyokuwa kumbukumbu ya kutolewa na Bwana toka utumwani Misri. Siku hii pia Wayahudi waliihusisha na kumbukumbu ya kupewa amri kumi na Mungu mlimani Sinai. Ilikuwa ni sherehe muhimu kwa wayahudi na walikusanyika Yerusalem kutoka pande zote waweze kuisherehekea pamoja. Katika siku hii, Mitume na wafuasi walikuwa bado wamekusanyika pamoja katika sala kama lilivyokuwa agizo la Kristo mwenyewe. Ndipo Roho Mtakatifu alipowatokea na kuwajaza wote nao wakaanza kuyatangaza matendo makuu ya Mungu, wakinena kwa lugha ambazo wageni wote waliokuja Yerusalem kwa sherehe walielewa kwa lugha zao wenyewe.

Katika somo hili tunaona kwanza, Roho Mtakatifu anajitambulisha kama Roho wa utulivu na umoja. Anawashukia mitume na wafuasi ambao walikuwa katika utulivu, wakiwa pamoja na wakisali pamoja. Ndivyo pia zama za Nabii Eliya (1Fal. 19:11-14), Bwana hakujitokeza kwake katika upepo unaopasua milima, wala katika tetemeko la nchi, wala katika moto bali katika sauti ndogo na upepo wa kisulisuli. Ndimi za moto ndiyo alama ya nje iliyoambatana na ujio wa Roho Mtakatifu kwa Mitume na kwa wafuasi. Na matokeo ya ujio wake ndiyo kuongea kwa lugha. Hawakunena mambo yasiyoeleweka wala mambo mengine yoyote bali walinena wakitanganza matendo makuu ya Mungu. Tayari hapa Roho Mtakatifu anadokeza atakachoendelea kutenda ndani ya watumishi wake, atawapa maneno ya kuongea kwa maana ni yeye atakayeongea kwa vinywa vyao na pia atawapa lugha na namna ya kuyanena kwa hao anaowakusudia.

Somo la Pili (1 Kor. 12:3b-7, 12-13) Mtume Paulo anazungumza juu ya karama na huduma mbalimbali walizonazo wanadamu na anaeleza kuwa zote hizo ni paji la Roho Mtakatifu. Asili yake ni Mungu mwenyewe na lengo lake ni kufaidiana, yaani kuwa faida kwa wengine; kuujenga mwili mmoja wa Kristo na kudhihirisha umoja wa mwili huo katika utendaji. Kama katika mwili viungo vipo vingi na hutegemeana ndivyo katika jumuiya karama zilivyo nyingi na hutegemeana.

Somo hili linakazia nafasi ya Roho Mtakatifu kama mgawaji wa karama na huduma. Hualika kwanza kila mmoja kutambua nafasi yake katika jumuiya, kutambua nafasi yake katika familia na hapo hapo huzialika jumuiya na familia kutambua nafasi na mchango wa kila mmoja anayeziunda, nafasi ambayo amepewa kama paji la Roho. Na kwa vile karama na huduma ni kwa ajili ya kufaidia na wala si kujifaidisha, somo linatualika kuweka ustawi wa jumuiya mbele katika kuziishi karama na huduma tulizojaliwa. Kuweka ustawi wa familia mbele. Kuwafikiria wengine kwanza na kuwapa nafasi ya kunufaika na uwepo wetu.

Injili (Yoh. 20:19-23) Kristo mfufuka anawatokea wanafunzi wake wakiwa bado wamejifungia kwa hofu ya wayahudi. Anawaambia “amani iwe kwenu”. Ni maneno ambayo ni zaidi ya salamu. Ni baraka ya Kristo Mfufuka kwa wanafunzi wake na ni urithi sasa anaowaachia; Amani. Kisha anawatuma. Anawatuma kama vile ambavyo yeye naye alitumwa na Baba. Anapowatuma, anawavuvia Roho Mtakatifu. Anawapulizia pumzi ya Roho Mtakatifu. Hapo Mwanzo wakati wa kuumbwa mwanadamu, Mungu alimpulizia pumzi ya uhai naye akafanyika mtu. Hapa kwa pumzi ya Roho Mtakatifu mwanadamu anapata uzima mpya, anaumbwa upya katika Roho. Ni hapa pia Kristo anaianzisha sakramenti ya Kitubio kwa kuwapa Mitume uwezo na mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi na mamlaka ya kuwafungia dhambi.

Tafakari fupi: Katika “Nasadiki” huwa tunaanza na maneno haya tunaposali kiri yetu kuhusu Roho Mtakatifu; “Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana na Mleta uzima atokaye kwa Baba na Mwana, anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana”. Ni maneno haya yanayotuambia Roho Mtakatifu ni nani. Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.  Anatoka kwa Baba na pia kwa Mwana kama tunda la upendo kati ya Baba na Mwana. Ana umungu mmoja sawa na Baba na sawa na Mwana ndio maana anaabudiwa kama anavyoabudiwa Baba na kama anavyoabudiwa Mwana. Roho Mtakatifu ni Mungu.

Sherehe ya Pentekoste, ni siku ambayo Roho Mtakatifu amefunuliwa kwa ukamilifu wake katika mpango wa Mungu wa wokovu kwa ulimwengu. Lakini Roho huyu amekuwapo tangu milele yote. Tukiangalia kwa ufupi tu tunaona kuwa katika uumbaji ulimwengu ulipokuwa bado tupu na giza ni Roho wa Mungu aliyekuwa juu ya vilindi vya maji. Ameshiriki katika uumbaji. Ndiye aliyewaongoza Waisraeli toka utumwani Misri kwenda nchi ya ahadi, mchana akiwa mbele yao kama wingu na usiku kama mnara wa moto: Ndiye aliyenena kwa vinywa vya manabii: katika umwilisho wa Nafsi ya Pili ya Mungu ndiye aliyemfunika Bikira Maria na kwa uwezo wake Neno wa Mungu akafanyika mwili ndani yake na hata Yesu mwenyewe alipoanza utume wake wa hadhara alijitambulisha kama aliye na Roho wa Bwana juu yake “Roho wa Bwana Mungu i juu yangu kwa maana amenitia mafuta kuwatangazia maskini habari njema”.

Ujio wa Roho Mtakatifu kwa Mitume ndio unaoashiria mwanzo wa utume wa Kanisa. Ndio kuzaliwa kwa Kanisa kwa maana tangu sasa wanatoka na kuanza kutekeleza utume walioachiwa na Kristo hadi hapo atakaporudi. Ndio utume ambao Kanisa linaufanya hadi leo. Linaufanya utume huo kwa nguvu za Roho Mtakatifu kwa maana Roho Mtakatifu ndio moyo (Mtima) wa Kanisa. Anafundisha Papa Pio XII ”Kristo ndiye Kichwa cha Kanisa na Roho Mtakatifu ndiye moyo wa Kanisa” (Mysici corporis, D. 2288).

Sisi nasi tunazaliwa katika maji na Roho Mtakatifu kwa ubatizo na tunapokea ukamilifu wa Roho Mtakatifu katika Sakramenti ya Kipaimara. Na hubaki ndani yetu akiishi kama katika hekalu. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu na tena tusimhuzunishe Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. Roho Mtakatifu anaendelea kutujia katika maadhimisho ya Sakramenti, katika kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu na kila tumwombapo kadiri ya mapenzi yake kwa maana “yeye huvuma kokote apendako”.

Tunamhitaji Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Yeye ni msaidizi wetu katika njia ya maisha na katika kila hatua zake zote; akitufundisha namna ya kusali, akituangaza kutenda yaliyo mema, akitupa nguvu ya kushinda vishawishi na mivuto ya ibilisi, akituinua katika madhaifu yetu na kutufariji tunapovunjika moyo. Kwa namna ya pekee zaidi tuombe neema ya kutambua utendaji wa Roho Mtakatifu katika umoja: umoja na familia, umoja na jumuiya, umoja na Kanisa. Tangu mwanzo Roho Mtakatifu amekuwa ni Roho anayeunganisha na si anayetenganisha, iwe ni kwa karama iwe ni kwa utendaji, iwe ni kwa namna ya kuishi na kushuhudia imani. Roho huyu aendelee kuliunganisha kanisa na kuunganisha ulimwengu mzima katika umoja alioukusudia. Nasi tuendelee mbele kwa imani na matumaini kuwa Roho Mtakatifu yuko nasi daima.

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS








All the contents on this site are copyrighted ©.