2018-05-18 15:16:00

Papa Francisko kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Pentekoste


Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. “Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana, Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana; aliyenena kwa vinywa vya Manabii.” Sherehe ya Pentekoste ni ukamilifu wa Fumbo la Pasaka ya Kristo na Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa katika ukamilifu wake. Pentekoste, inawafanya Wakristo wote kuwa ni sehemu ya watu wa Mungu, taifa lake jipya na teule, yaani Kanisa.

Ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu watoto wa Mungu wanaweza kuzaa matunda. Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Sherehe ya Pentekoste ni maadhimisho ya kuzaliwa kwa Kanisa. Kwa ufupi tunaweza kusema, Pentekoste ni sherehe ya mwanzo wa Agano Jipya lililofungwa kwa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni mwanzo wa Taifa jipya la Mungu lililojaa Roho wake Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Jumapili, tarehe 20 Mei 2018 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada ya Misa Takatifu itaanza saa 4:00 kwa saa za Ulaya. Baadaye, Baba Mtakatifu atatoa tafakari yake wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, inayofunga rasmi kipindi cha Pasaka, tayari, waamini kutoka kifua mbele kwenda kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, kama sehemu muhimu sana wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Sala hii itukumbushe wajibu na dhamana hii nyeti: “Ee Mungu, wewe unalitakasa Kanisa lako lote lililo kati ya makabila na mataifa yote kwa Fumbo la Sherehe ya Pentekoste. Eneza mapaji ya Roho Mtakatifu popote duniani; na zile karama ulizozitoa tangu mwanzo wa kuhubiriwa Injili, hata sasa uzieneze kwa juhudi ya waamini wako. Amina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.