2018-05-17 17:00:00

Papa Francisko apokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 17 Mei 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wasio wakazi wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican. Balozi hawa wanatoka Tanzania, Lesotho, Pakistan, Mongolia, Denmark, Ethiopia na Finland. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaomba mabalozi kuwafikishia wakuu wao wa nchi pamoja na raia wao, salam na matashi yake mema na kwamba, anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Diplomasia ya Kimataifa ni kazi ambayo inahitaji uvumilivu mkubwa ili kukuza na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu kwa kutambua kwamba, umoja wa familia ya binadamu unafumbatwa katika utu na heshima ya binadamu.

Kutokana na mwelekeo huu, diplomasia ya Kanisa inalenga zaidi maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ili kukuza na kudumisha majadiliano, ushirikiano pamoja na huduma kwa ajili ya mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa mwaka 2018 inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa Tamko la Haki Msingi za Binadamu, changamoto na mwaliko wa kukuza na kudumisha mshikamano baina ya watu wa Mataifa katika mapambano dhidi ya umaskini, magonjwa, dhuluma na nyanyaso.

Wanadiplomasia wanao wajibu wa kimaadili wa kupambana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Kuna haja ya kusikiliza na kutoa majibu muafaka ya changamoto zinazoibuliwa kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hiki ni kipindi maalum cha mabadiliko makubwa yanayohitaji kwa namna ya pekee, hekima na mang’amuzi ili kujenga jamii inayosimikwa katika amani na maendeleo endelevu hata kwa kizazi kijacho.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba mabalozi wapya wanaoziwakilisha nchi zao, wataweza kukuza na kudumisha ushirikiano na ushiriki mkamilifu katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Kanisa kwa upande wake, linataka kukuza na kudumisha majadiliano kwa kuwajibikiana; kukuza ari na mwamko wa kushirikiana, pasipo ujeuri wala udanganyifu ili kuujenga ulimwengu katika udugu na amani ya kweli. Changamoto kubwa kwa wakati huu mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowakirimia, watu hawa wanaokimbia vita na baa la njaa au wanalazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na ubaguzi, dhuluma, nyanyaso, umaskini au uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni wajibu wa kimaadili unaovuka mipaka, kisingizio cha usalama wa raia na mali zao na mafao ya nchi binafsi. Licha ya changamoto changamani na hali tete ya kisiasa na kijamii inayogubikwa katika mazingira kama haya, mataifa binafsi na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake inachangamotishwa kukuza na kudumisha amani na upatanisho; kwa kuzingatia maamuzi yanayofumbatwa katika huruma, ujasiri pamoja na kujiwekea malengo ya muda mrefu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka Mabalozi wapya pamoja na kuwahakikishia ushirikiano wa dhati kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican, ili kuwarahisishia utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kidiplomasia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.