2018-05-10 14:12:00

Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza Wafokolari!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha hija yake ya kichungaji kwenye Jumuiya ya Nomadelfia, Alhamisi, tarehe 10 Mei 2018, aliondoka na kuelekea mjini Loppiano ambao kwa mara ya kwanza katika historia yake, umepata bahati ya kutembelewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Kanisa ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, Theotokos. Akapa nafasi ya kusikiliza salam kutoka kwa Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha Kitume cha Wafokolari na baadaye, Baba Mtakatifu Francisko akazama katika maongezi na wananchi wa mji wa Loppiano unaosimikwa katika kifungo cha upendo na umoja kwa kujibu maswali makuu matatu!

Hii ni hija ambayo imeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za wananchi wa Loppiano kwani ni mji ambao unapata chimbuko lake kutoka katika Injili, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa wafuasi wa Kristo pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kati ya watu. Hapa ni mahali ambapo, watu wengi wanajisikia wako nyumbani. Ni mji ambao ulianzishwa na Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich aliyetaka kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika huduma kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto inayotolewa na Roho Mtakatifu hata kwa familia ya Mungu nyakati hizi.

Wananchi wa mji wa Loppiano, tangu mwanzo wameyasimika maisha yao katika Amri ya upendo kama chemchemi ya maisha ya Kikristo! Katika kipindi cha miaka 50, sasa wanakabiliana na changamoto mpya, ndiyo maana wanamwomba Baba Mtakatifu awapatie neno litakaloweza kuwasaidia kuendelea kumwilisha ushuhuda wa kinabii, uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa mji huu. Baba Mtakatifu anawashukuru wanachama Wafokolari kwa kuacha yote na kuambata changamoto za Kiinjili ili kumwilisha imani yao kwa Kristo Yesu katika matendo.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kuendeleza upya wa maisha kama unavyodadavuliwa kwenye Waraka kwa Waebrania kwamba, kwa njia ya nuru walistahimili mashindano makubwa ya maumivu, wakashinda shutuma na dhiki; wakaonesha moyo wa ushirikiano, umoja na huruma kiasi hata cha kukubali kunyang’anywa mali zao kwa kutambua thawabu kubwa iliyokuwa nyoyoni mwao. Baba Mtakatifu anasema, bado wanahitaji ujasiri na saburi katika kutekeleza mapenzi ya Mungu.

Maandiko Matakatifu yanakazia kwa namna ya pekee, mtindo wa maisha ya wafuasi wa Yesu unaojikita katika: ushuhuda wa ukweli, imani, matumaini na uchaji wa Mungu ili kutangaza na kushuhudia matendo ya makuu ya Mungu katika maisha yao! Hii ni zawadi ambayo wanapaswa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia, ili kukuza na kudumisha ukweli, uwazi, ujasiri na upendo. Mtume Paulo anawataka waamini hata katika dhidi kufurahi, kwani dhidi kazi yake ni kuleta saburi na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini ambalo kamwe halitahayarishi kwa maana tayari wamekwisha kumiminiwa upendo wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka Wafokolari kujikita katika ule upendo wa kwanza, uliopelekea hata Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich kuanzisha Jumuiya ya Loppiano. Akataka Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza kwa njia ya sala na Ibada ya Ekaristi Takatifu, chemchemi ya umoja, upendo, udugu na mwanga katika mchakato wa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili katika jamii, changamoto endelevu iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Karama ya umoja ikawa ni chemchemi ya ari na mwamko wa Injili mjini Loppiano. Hiki ni kielelezo cha umoja na utofauti unaofumbatwa katika maisha ya wanajumuiya wake, ili kwa pamoja waweze kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kumwilisha tunu msingi za Kiinjili na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwatangazia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Lengo kuu ni umoja wa watoto wa Mungu unaofumbatwa katika upendo wa Mungu na jirani sanjari na kukazia mambo msingi katika maisha!

Katika maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kitume cha Wafokolari, wanapaswa kujikita zaidi katika ujenzi wa Jumuiya ambayo kweli watu wanajisikia kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na watu wake sanjari na kuendeleza mchakato wa malezi na majiundo makini ya watu. Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la pili amewataka Wafokolari kumtumainia Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu, kwa kusikilizana na kushirikiana karama ili kujenga na kudumisha umoja. Majiundo makini katika maisha ya kiroho, miito mbali mbali, kiuchumi na kisiasa. Majiundo yakazie majadiliano ya kidini na kiekumene; Kikanisa na kitamaduni kwa ajili ya huduma kwa binadamu.

Majiundo yote haya yajikite katika umoja wa familia ya Mungu, ili kukuza ujirani mwema na majadiliano yanayobubujika kutoka: akilini, moyoni na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Majiundo haya yawe ni utambulisho wa maisha na uwepo wao. Chuo Kikuu cha Sophia ambacho kinatambuliwa na Vatican na sasa kinaendelea kupanuka hata huko Amerika ya Kusini ni mahali muafaka pa kujichotea hekima itakayosaidia kujenga utamaduni wa umoja; kwa kujikita katika masomo yatakayotoa mchango mkubwa ili kuliwezesha Kanisa kufanya mabadiliko katika ari na moyo wa kimisionari unaokazia umoja wa watu wa Mungu.

Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich katika kipindi cha miaka 50 ya uwepo na utume wa Wafokolari amekazia mji wa Loppiano kuwa ni kitovu cha Injili, Shule, Mlima wa furaha, majadiliano na kwamba, huu ni mji wa Bikira Maria Mama wa Mungu. Changamoto kubwa iliyoko mbele yao kwa wakati huu ni umwilishaji wa utume wa Loppiano katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la tatu kuhusu jinsi ya kukabiliana na changamoto mamboleo, amewataka wanachama hawa kuwa na imani na matumaini, waendelee kujikita katika uaminifu kwa kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, ili kuhakikisha kwamba, mji wa Loppiano unazamisha mizizi ya historia katika huduma, ushuhuda na umwilishaji wa tunu msingi za Kiinjili katika unyenyekevu, ukweli, uwazi na uthubutu!

Daima wajiaminishe katika neema ya Mungu, ili kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu mbali mbali, ili kudumisha utamaduni wa utandawazi wa agano linalofumbatwa katika upendo wa Mungu. Ili kufanikisha azma hii, kunahitajika umoja na mshikamano wa watu wote wa Mungu. Changamoto kubwa mbele yao ni uaminifu mbunifu unaowawezesha wanajumuiya hii kujiaminisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, daima wakijitahidi kupambanua sera na mikakati yao kwa njia ya kijumuiya, ili wote waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa mang’amuzi ya kijumuiya.

Baba Mtakatifu Francisko anasema mbele ya Kanisa la Madhabahu ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, kuna kumbu kumbu endelevu ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Karama ya Wafokolari ambao kimsingi wanatambua kwamba, Kanisa ni Kazi ya Bikira Maria. Tarehe 21 Novemba 1964 Mwenyeheri Paulo VI alimtangaza Bikira Maria kuwa ni Mama wa Kanisa. Na kwa mara ya kwanza Siku kuu hii itaadhimishwa Jumatatu, tarehe 2 Mei 2018 baada ya Sherehe ya Pentekoste. Bikira Maria ni Mama wa Kristo, Mama wa Kanisa na Mama wa wote, mwaliko kwa waamini kujiaminisha kwenye “Shule ya Bikira Maria” ili kujifunza namna ya kumfahamu Kristo Yesu, kuishi naye na kutambua uwepo wake kati ya watu wanaowazunguka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.