2018-05-09 16:25:00

Papa Francisko anatembelea Nomadelfia na Loppiano nchini Italia


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 10 Mei 2018 anafanya hija ya kichungaji huko Toscana, ambapo ataanzia Nomadelfia na hapo atapokewa na Askofu Rodolfo Cetoloni wa Jimbo Katoliki la Grosseto, Padre Ferdinando Neri, na Francesco Matterazzo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nomadelfia. Huko atapata nafasi kwenda kusali katika kaburi la Don Zeno Saltini, na baada ya kuonana na wanajumuiya wa Nomadelfia, na atakuwa na tafrija na vijana wa jumuiya hiyo, ambapo atazungumza nao mawili matatu.

Askofu Cetoloni anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu huko Nomadelfia imekuja kwa wakati wake, muda mfupi tu, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuchapisha Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) ambamo anakazia umuhimu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha katika maisha yao “Heri za Mlimani” ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, hasa kwa kukazia umuhimu wa kusamehe wale waliowakosea kwa kutambua kwamba, hata wao, wanahitaji msamaha wa dhambi zao na huruma ya Mungu.  Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kupata furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Bwana Francesco Matterazzo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nomadelfia anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu huko Nomadelfia ni kielelezo kwamba, Kanisa linatambua utakatifu wa Don Zeno Saltini, aliyeanzisha Jumuiya hii kunako mwaka 1947, huko karibu na mji wa Grosseto. Ni Padre alionesha upendo mkubwa kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; ni kiongozi aliyesimika maisha yake katika fadhila ya utii, imani na matumaini, akapambana na maisha, huku akijiaminisha kwa ulinzi na tunza ya Kristo Yesu. Jumuiya hii imekuwa na uhusiano mzuri na viongozi wa Kanisa kuanzia na Papa Pio XII, Mwenyeheri Paulo VI pamoja na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea huko kunako mwaka 1989 ili kujionea Utume wa familia, akabatiza mtoto mchanga na kuzungumza na bahari ya watu waliofika kumsikiliza.

Utume wa Familia ni Jumuiya ya wanawake wanaolea na kukuza miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Hawa ni wanawake ambao bado hawajaolewa lakini wanajitoa na kujisadaka kwa ajili ya malezi na majiundo kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi, wazee pamoja na wagonjwa. Kuna umati mkubwa wa akina mama wanaobahatika kupata watoto, lakini kwa bahati mbaya kutokana na hali na maisha yao, wanashindwa kuwalea na kuwahudumia vyema watoto wao.

Baba Mtakatifu Francisko anatembelea “Shule Hai” iliyoanzishwa na  Don Zeno inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Shule hii kwa sasa inaongozwa na  Maria Izzo inahudumia watoto wenye umri kati ya miaka 12-15. Watoto hawa wanapewa elimu makini inayowashirikisha hata wazazi wao katika kufanya maamuzi mbali mbali. Lengo ni kumhudumia mwanadamu katika asili yake kama alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu. Shule hai kadiri ya mipango, sera na mikakati ya Don Zeno ilikuwa ni kumpatia fursa kijana kuishi kikamilifu na kuendelea na masomo yake katika mazingira ya maisha ya kijumuiya. Hapa vijana wanafundwa elimu dunia na maisha ya kiroho, ili kweli waweze kuwa raia wema na watakatifu.

Vijana wanafundwa pia kutambua na kuheshimu umuhimu wa kazi za mikono zinazowasaidia kujitegemea na kuitegemeza jumuiya yao. Hapa kijana anasaidiwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji. Bwana Francesco Matterazzo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nomadelfia anakaza kusema, Jumuiya hii inawasaidia watu kumtambua Mwenyezi Mungu na hivyo kuweza kushiriki kikamilifu kwa kushirikiana na jirani zao wote, Hawa ni waamini wanaomwilisha katika maisha na utume wao, Injili ya upendo wa Kristo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko, itasaidia kuimarisha imani, matumaini na mapendo ya wanajumuiya ya Nomadelfia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.